Dar es Salaam. Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imesema, kwa kipindi cha miaka mitano, wanafunzi 15,003 waliokatiza masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito, wamesajiliwa kujiunga na programu za elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi wa elimu.
Kufuatia hatua hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Daniel Mushi amesema wizara hiyo itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha watoto waliokatiza masomo ya elimu ya sekondari wanarejeshwa na kupata nafasi ya kuendelea na elimu kupitia taasisi hiyo.
Utekelezaji huo ni agizo alilowahi kutoa Rais Samia Suluhu Hassan Novemba 24, 2021, akieleza msimamo wa Serikali kuruhusu kurejea shuleni kwa wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwamo ujauzito.
Hatua hiyo ilifuatiwa na mwongozo uliotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Februari 2022 ukilenga kutoa fursa ya pili kwa wanafunzi waliokatishwa masomo ili waweze kuendelea na elimu ili kufikia ndoto zao.
Akizungumza Desemba 17, 2025 katika mahafali ya 64 ya TEWW, Profesa Mushi alisema kupitia programu ya elimu changamani inayotekelezwa na taasisi hiyo wanafunzi wanajengewa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na jamii.
“Hatua hii ni muhimu kwa kudumisha matokeo chanya yaliyokwisha kupatikana hadi sasa na kuendeleza dhamira ya serikali ya kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma katika safari ya elimu,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Daniel Mushi
Profesa Mushi alisema dhamira ya Serikali kupitia ni kuhakikisha elimu inakuwa chombo cha kuwezesha wananchi kujitegemea, kuimarisha uchumi, kupunguza umasikini na kuleta usawa wa kijamii.
Kwa upande wake Mkuu wa TEWW, Profesa Philipo Sanga alisema TEWW imeendelea kusimamia utolewaji wa elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi na kuboresha miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji.
“Mwaka huu pekee tumesajili jumla ya wanafunzi 5,977 wanaume 4,180 wanawake 1,797) ndani ya vituo takribani 192 vilivyopo nchi nzima.
“Katika kipindi cha miaka mitano wanafunzi 15,003 wameweza kurejeshwa shule baada ya kukatiza masomo kwa sababu mbalimbali,” alisema.
Profesa Sanga alisema kupitia mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya Sekondari (SEQUIP), TEWW imejenga majengo 13 yenye vyumba vya madarasa na vyumba vya kuelelea watoto.
Akizungumzia mahafali hayo, alisema jumla ya wanafunzi 2331 wametunukiwa ngazi mbalimbali za elimu.
Kwa upande wake, rais wa serikali ya wanafunzi wa taasisi hiyo, Aloyce Joseph amewapongeza wahitimu hao kuvumilia hadi kuhitimu mafunzo akiwasisitiza wakufunzi wamekuwa nguzo muhimu ya kutimiza ndoto ya wanafunzi.
“Maarifa mliyoyapata yawe msingi wa uadilifu na chachu ya maendeleo kokote mwendako kwani Taifa linawategemea katika kutatua changamoto zilizopo kwa kutumia ujuzi mlioupata,” alisema.
Mwakilishi wa wahitimu Paul Monka elimu waliyopata watatumia kuijenga jamii na kuwa wazalendo kwa Taifa.
