Vatican. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo, amelaani tabia ya baadhi ya viongozi wa dini kutumia mamlaka na ushawishi wao kwa waumini kuhalalisha migogoro na migawanyiko ndani ya mataifa yao.
Leo, ambaye ni Papa wa kwanza kutoka nchini Marekani, ameyasema hayo kupitia ujumbe wa kurasa nne uliotolewa kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani ya Kanisa Katoliki, yanayolenga kusisitiza umuhimu wa kulinda, kuimarisha, na kudumisha amani katika jamii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Desemba 18, 2025, Papa Leo amesema kumekuwa na baadhi ya viongozi wa dini wanaotumia kigezo cha sera za uzalendo, kama nyenzo ya kupandikiza chuki miongoni mwa waumini kitendo ambacho amekiita ni kufuru, au dhambi kubwa inayomdharau na kumtukana Mungu.
“Kwa bahati mbaya, imekuwa jambo la kawaida zaidi kuivuta lugha ya imani katika vita vya kisiasa, kubariki utaifa, na kuhalalisha vurugu na mapambano ya silaha kwa jina la dini,” amesema Papa.
Amesema waumini lazima wajue kukanusha kikamilifu, mafundisho na maelekezo yote ya viongozi wa dini ambao wamekuwa na tabia hii, ili kuondoa uwezekano wa kutokea kwa migogoro ndani ya Taifa.
Kiongozi huyo pia ameonya matumizi ya akili bandia katika vita ambazo zinaendelea baina ya mataifa mbalimbali ulimwenguni ikiwemo Russia na Ukraine.
Amesema matumizi hayo yanaongeza kiu kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa na kijeshi kukwepa uwajibikaji, huku maamuzi kuhusu uhai na kifo yakizidi kukabidhiwa kwenye teknolojia hizo.
Kwa mujibu wa Papa hali inayoashiria usaliti usio wa kawaida na uharibifu wa kanuni za kisheria na kifalsafa za ubinadamu ambazo ndizo msingi na kulinda kila ustaarabu.
Katika ujumbe huo Papa pia alilalamikia ongezeko la matumizi ya kijeshi duniani, akitoa mfano wa takwimu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Kimataifa ya Stockholm kwamba matumizi ya kijeshi duniani kote yameongezeka.
Papa Leo, aliyeteuliwa na Makardinali kutoka mataifa mbalimbali Mei kumrithi marehemu Papa Francis, amekuwa akizungumzia mara kadhaa changamoto na athari zinazotokana na matumizi ya Akili Unde (AI).
Imeandaliwa na Elidaima Mangela
