Dar es Salaam. Serikali iko kwenye mkakati wa usimamiaji wa biashara mtandaoni ikiwa ni moja ya njia inayolenga kuleta mageuzi ya biashara kidijitali.
Makakati huo unaandaliwa ili kuendana na kasi ya ukuaji wa maendeleo ya teknolojia ambayo yamechochea kuibuka na kukua kwa biashara mtandao.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Desemba 18, 2025 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Kapinga amesema hadi mwaka 2024 kampuni na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao kupitia biashara mtandao zilizosajiliwa zilikuwa 1,820.
Ili kuwezesha hilo, Serikali inaendelea kuchukua hatua muhimu za kuwa na mfumo madhubuti utakaosimamia biashara hiyo na mkakati wa kitaifa wa biashara mtandao unaandaliwa.
“Mkakati unaondaliwa utajumuisha nafasi ya vijana katika biashara hiyo kwa upekee. Serikali inaona nguvu ya vijana kama sehemu muhimu ya maendeleo ya Taifa.
Tutaendelea kuweka na kubuni miundombinu, mafunzo na rasilimali ili biashara mtandaoni iwe rahisi kwa vijana. Tutawahakikishia malipo salama, masoko makubwa na msaada wa kitaaluma,” amesema.
Ili hilo lifanikiwe, vifaa na teknolojia vitapatikana karibu ili kila kijana awe na fursa ya kufanikisha ndoto zake.
“Tutahimiza ubunifu na changamoto zinazotoa zawadi, kuifanya biashara mtandaoni iwe burudani na faida. Kwa pamoja, vijana na Serikali tutaijenga Tanzania yenye wajasiriamali hodari, wenye bidhaa zinazoshindana kimataifa hili ndiyo lengo letu na tutafanikisha hayo,” amesema.
Mbali na kuwezesha biashara mtandaoni, pia Kapinga amesema Serikali itaendelea kuongeza uwezo wa taasisi za fedha ili kutoa mikopo kwa vijana wanaotaka kuanzisha viwanda vidogo, biashara za uzalishaji na ubunifu wa teknolojia.
Amesema kwa sasa mfuko ulio chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wajasiliamali ni ule wa NEDF ambao umewezesha mikopo 841 yenye thamani ya Sh2.4 bilioni.
Wakati huo pia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TaDB) imetoa mikopo ya Sh54.24 bilioni kwa viwanda vya mazao na mfuko wa dhamana umetoa Sh11.96 bilioni kwa viwanda 26.
“Mikopo hii ni ya riba nafuu ambayo ni chini ya soko (asilimia 9). Aidha, benki za NMB, CRDB na nyingine wanatoa mikopo yenye riba nafuu kwa wajasiliamali ya mpaka asilimia 9,” amesema.
Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Humprey Mushi amesema ili yote yaliyokusudiwa yafanyike, ni vyema kuhakikisha mipango inayowekwa inatengenezewa mikakati ikiwamo kufanyiwa ufuatiliaji kuangalia kile kilichokuwa kimekusudiwa kimefanyika kwa kiwango gani, fursa gani nyingine zilizojitokeza, namna nchi inavyoweza kujipanga.
“Kila wakati iwe ni kazi ya wizara na watu wake na wataalamu kutoka maeneo mbalimbali, kama suala la kuuza nje ni vyema kushirikisha sekta binafsi wakae walau mara tatu wazungumze na hata baraza la biashara la Taifa lishirikishwe kikamilifu,” amesema.
Pia, ametaka kuwekwe mazingira mazuri ya uwekezaji kwa ajili ya kuvutia mitaji huku msingi mkubwa wa kufanikisha hilo likiwa ni kuhakikisha amani na utulivu inazingatiwa kwa kuwa, ikipotea hakuna mtu atakuja kuwekeza.
“Maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanategemea amani,” amesema.
Mkakati kukuza biashara za nje
Mbali na biashara mtandao pia Tanzania iko katika hatua za mwisho za uandaaji wa mkakati wa mauzo nje ya nchi utakaowajumuisha vijana katika utekelezaji wake.
Mkakati huo unalenga kuwezesha ufikiaji wa fursa ya kupata masoko bora ya bidhaa ambayo Tanzania ni mwanachama ili kusaidia kukuza uchumi wa Taifa na mtu mmoja mmoja.
Akizungumzia mkakati huo, Kapinga amesema mpaka sasa Tanzania inauza bidhaa zake katika masoko ya Asia, Umoja wa Ulaya, Soko Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) huku akibainisha kuwa, uwepo wa masoko hayo na mengine tunayoendelea kuyatafuta, unatupa fursa ya kupanua wigo kuuza baishara nje.
“Kwa sasa tupo katika hatua za mwisho za uandaaji wa mkakati wa mauzo nje ya nchi ambao utawajumuisha vijana katika utekelezaji wake. Tunataka moja wapo ya kundi litakalokuwa linanufaika na fursa ya kupata masoko bora ya bidhaa basi liwe ni kundi la vijana. Na hivyo, tutahakikisha mkakati huu unakua jumuishi,” amesema Kapinga.
Ili nchi iweze kushikiri katika biashara kikamilifu yapo masuala ya kuyafanyia kazi ikiwamo kuongeza nguvu kubwa katika kurasimisha biashara, kuendelea kuboresha mifumo ya kidigitali ili wawekezaji na wafanyabiashara wapate huduma za kufungua na kuenndeleza biashara zao kwa urahisi.
“Tumeshafanyia kazi urahisi wa kurasimisha biashara na kusajili biashara japokuwa bado kuna masuala ya kuendelea kuboresha ikiwamo kuhakikisha taasisi zetu zinakuwa wezeshi na sio udhibiti na pia tukimkuta mtu hana leseni hatufungii biashara bali tumsaidie arasimishe biashara, tunapanua wigo mapato,” amesema Kapinga.
Hili linafanyika wakati ambao sekta ya viwanda ilichangia asilimia 7.3 ya Pato la Taifa katika mwaka 2024, ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2023 wakati ambao ukuaji wa sekta yenyewe ukiongezeka kutoka asilimia 4.3 mwaka 2023 hadi asilimia 4.8 mwaka 2024.
Kwa upande wa sekta ya biashara, mchango wake katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 8.4 mwaka 2023 hadi asilimia 8.6 mwaka 2024, huku kasi ya ukuaji ikipanda hadi asilimia 4.8.
“Ongezeko hili limetokana na maboresho makubwa kwenye mazingira ya biashara, upanuzi wa viwanda vinavyoongeza lakini pia na juhudi za Serikali kufungua masoko mapya ya kikanda na kimataifa,” amesema Kapinga.