Na Pamela Mollel,Arusha
Meya wa Jiji la Arusha, Mheshimiwa Maximilian Matle Iranghe, ametoa tathmini ya ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mheshimiwa Riziki Shemdoe, iliyofanyika mkoani Arusha kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Jiji la Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 18, 2025, ofisini kwake, Meya Iranghe amesema ziara hiyo imelenga kupata picha halisi ya hatua za utekelezaji wa miradi pamoja na changamoto zinazojitokeza, hatua inayoiwezesha Serikali kutoa maelekezo ya haraka na sahihi kwa ajili ya kuboresha utekelezaji wake.
Ameeleza kuwa miongoni mwa miradi iliyokaguliwa ni ujenzi wa uwanja wa mpira pamoja na ujenzi wa soko jipya, miradi ambayo ni muhimu katika kukuza sekta ya michezo, biashara na kuchangia ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Jiji la Arusha.
Kwa mujibu wa Meya Iranghe, Waziri wa TAMISEMI ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo na kusisitiza kuwa hakuna sababu ya kuongeza muda wa utekelezaji wa miradi iliyopangwa. Waziri amewaelekeza wakandarasi na wasimamizi kuhakikisha wanazingatia viwango vya ubora na kukamilisha miradi kwa wakati uliopangwa.
Aidha, Meya Iranghe amebainisha kuwa ziara za viongozi wakuu wa Serikali zina mchango mkubwa katika kuongeza uwajibikaji kwa watendaji na kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mamlaka za serikali za mitaa.
Katika hitimisho lake, Meya Iranghe ameishukuru Serikali Kuu pamoja na wizara husika kwa kuendelea kutoa ushirikiano na ufuatiliaji wa karibu, akisisitiza kuwa Jiji la Arusha litaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa manufaa ya wananchi.
