Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imeamuru kuachiwa huru kwa Mkurugenzi wa FX Bureau De Change, Faruk Osman Sidik aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha.
Badala yake, Mahakama hiyo imeelekeza mlalamikaji katika shauri hilo, Roshanal Abdulrasul Moledina kufungua kwanza shauri la madai kama kifungu cha 4(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) R.E 2023 kinavyoelekeza.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 16141 ya mwaka 2025, alikuwa anakabiliwa na mashitaka mawili, kosa la kwanza ikiwa ni kujipatia fedha kwa njia ya uongo Sh3.4 bilioni kutoka kwa Moledina, ili ampatie Dola za Marekani.
Kulingana na maelezo hayo, kosa hilo lilidaiwa kutendeka kati ya Agosti 28,2018 na Novemba 2,2018 katika Mtaa wa Samora Jijini Dar es Salaam, Sidik alipokea fedha hizo kutoka kwa Moledina ili ampe Dola 1,550,000 za Marekani.
Katika kosa la pili, ilidaiwa katika tarehe hizohizo, mfanyabiashara huyo alijipatia Sh3.4 bilioni kutoka kwa Moledina huku akijua kuwa wakati anazipokea zilikuwa ni za uhalifu lililotokana na kujipatia fedha kwa njia ya uongo.
Uamuzi wa kumwachia huru Sidiki maarufu ‘Sadick’, umetolewa Desemba 17,2025 na Jaji Sedekia Kisanya wakati akitoa uamuzi mdogo kuhusiana na pingamizi lililowasilishwa na mawakili waliokuwa wakimtetea mfanyabiashara huyo.
Jaji Kisanya alitoa uamuzi huo kuhusiana na pingamizi la awali lililowasilishwa na mawakili waliokuwa wakimtetea mfanyabiashara huyo, Alex Mgongolwa, Oscar Magolosa na Moses Kimaro, waliosema kesi hiyo ina viashiria vya madai.
Baada ya Jamhuri kusoma taarifa ya namna kosa hilo la uhujumu uchumi lilivyotendeka, mshitakiwa ambaye mbali na kuwa mkurugenzi lakini ana hisa katika duka hilo la kubadilisha fedha, alikanusha makosa yote mawili.
Jamhuri iliishitaki FX Bureau De Change kama mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo.
Baada ya kukana shitaka, kesi hiyo ilianza kwa upande wa mashitaka kuleta shahidi mmoja na ikaahirishwa lakini ilipoendelea Novemba 11,2025, mawakili wa mfanyabiashara huyo wakawasilisha pingamizi kuwa maelezo yaliyokuwa yamesomwa, yanakiuka kifungu hicho cha 4(3) cha CPA kama kilivyorekebishwa 2023.
Wakili Mgongolwa katika hoja zake, alisema maelezo ya mlalamikaji yanaonyesha alimfuata mshitakiwa kwa lengo la kununua Dola za Marekani, na wakakubaliana kuwa mlalamikaji angewasilisha shilingi za Tanzania ili ambadilishie kwenda Dola.
Alieleza kuwa makubaliano hayo yana sura ya kimkataba hivyo mlalamikaji alikuwa anataka nguvu ya kutekelezwa kwa makubaliano hayo na kurejea kifungu cha (2)1(h) cha sheria ya mikataba Sura ya 345 kama ilivyofanyiwa marejeo 2023.
Wakili Mgongolwa alisema hata maelezo ya shahidi wa mlalamikaji aitwaye Riyaz Mohamed Hussein, yanaunga mkono juu ya uwepo wa makubaliano hayo.
Kwa mujibu wa wakili huyo, makubaliano ya aina hiyo yanaweza kusukumwa utekelezaji wake kupitia mashauri ya madai na kifungu cha 4(3) cha CPA kinataka kunapokuwa na mazingira hayo, nafuu ya madai ishughulikiwe kabla ya jinai.
Wakili Mgongolwa alisema hata maelezo ya Neema Waiton Nyazi ambayo yanathibitisha kuwa mshitakiwa wa pili ambaye ni FX Bureau De Change anajishughulisha na biashara ya kubadilisha fedha, hivyo kunapotokea wamekiuka jambo lolote baya, basi linaangukia katika ukiukwaji wa mkataba.
Alisema kwa kuegemea kumbukumbu za mahakama, suala hilo linaweza kuamuliwa bila usikilizwaji wa shauri la msingi la jinai kwa kuwa taarifa ya kosa inakiuka kifungu cha 4(3) cha CPA hivyo akaomba mteja wake aachiwe huru.
Akijibu hoja hiyo, wakili Mwandamizi wa Serikali, Edgar Bantulaki aliyekuwa anasaidiana na Patrick Mwita, alipinga hoja za upande wa utetezi akisema pingamizi hilo limewasilishwa kabla ya wakati.
Alidai kuwa hoja hiyo imeegemea katika maelezo ya mashahidi ambao ni ushahidi wa nyaraka uliosomwa wakati wa mwenendo kabidhi (commital) na bado zilikuwa hazijatolewa kortini na kupokelewa kama vielelezo na mahakama.
Wakili Bantulaki alisema mwenendo wa kabidhi unafanyika chini ya kifungu cha 260 na 264 cha CPA na lengo lake ni kusaidia maandalizi ya usikilizwaji wa kesi ili pande zote mbili ziweze kujua nini kinajenga msingi wa kesi hiyo ya jinai.
Kuhusu kifungu cha 4(3) cha CPA, wakili Bantula alisema hakitumiki kwa makosa yanayoangukia chini ya Kanuni ya Adhabu na kusisitiza kosa la kujipatia fedha kwa njia ya uongo linaangukia nje ya kifungu hicho cha 4(3).
Katika uamuzi wake, Jaji Kisanya alisema baada ya kupitia kwa umakini kumbukumbu za mahakama na mawasilisho ya mawakili wa pande mbili, mahakama yake inaalikwa kuamua kama taarifa ilikiuka kifungu cha 4(3).
Alinukuu kifungu hicho cha 4(3) kinachosema pale ambapo shauri lina uasili wa kimadai, kiutawala au jinai, basi mahakama itashughulikia kwanza nafuu ya kimadai kabla ya suala hilo kushughulikiwa kwa njia ya jinai.
Jaji Kisanya alisema kwa kuangalia kifungu hicho, kinabainisha kuwa Bunge lilitambua mgogoro unaweza kuibuka ndani ya nyanja za kisheria zinazoingiliana, madai, utawala na jinai na kitaka nafuu ya madai ishughulikiwe kabla ya jinai.
“Dhamira ya watunga sheria chini ya kifungu cha 4(3) cha CPA ni kuhakikisha kuwa mchakato wa jinai hautumiwi kama njia ya awali ya kushughulikia migogoro ambayo iko ndani ya uwanja wa kiraia au utawala,” alisema Jaji Kisanya.
Alisema katika kesi hiyo, pingamizi liliibuliwa katika hatua ambayo upande wa mashitaka ulikuwa tayari umeleta shahidi mmoja na ulikuwa bado haujaita mashahidi muhimu akiwamo mlalamikaji katika kesi hiyo.
Baada ya kupitia maudhui yaliyowasilishwa wakati wa ukabidhi na pia ushahidi uliosomwa wakati wa usikilizwaji wa awali, Jaji alisema ni dhahiri kuwa Moledina alimfuata mshitakiwa kwa dhamira ya kununua Dola 1,550,000 za Marekani.
“Ushahidi wote unaotarajiwa na maelezo yaliyosomwa yanaonyesha mlalamikaji na mshitakiwa walikubaliana kwamba mlalamikaji angepeleka shilingi za Tanzania na mshitakiwa angezibadili na kuwa katika Dola ya Marekani,” alisema Jaji.
Jaji alisema maelezo hayo yanaonyesha wazi kuwa makubaliano hayo yanatoa vigezo kuwa kulikuwa na mkataba kama inavyoelezwa katika sheria ya mikataba na malalamiko ya mlalamikaji yanatokana na mshitakiwa kutotimiza makubaliano.
Katika kufafanua zaidi suala hilo, Jaji alinukuu maelezo ya mlalamikaji yanayoonyesha kuwa ulipofika msimu wa kilimo alimfuata mshitakiwa ili ampe Dola kama walivyokubaliana, lakini akamjibu duka lilifungwa na pesa zote zilichukuliwa na Serikali lakini baadaye alipata taarifa kuwa alirudishiwa.
Jaji alisema kwa kutazama ushahidi huo unaotarajiwa kuletwa na Jamhuri ni wazi unaangukia katika mkataba ambayo ni suala la madai na sio jinai.
Ni kutokana na uchambuzi huo, Jaji alikubaliana na pingamizi lililowasilishwa na upande wa utetezi hivyo taarifa iliyowasilishwa na Jamhuri inaondolewa na mshitakiwa anaachiwa, ingawa hilo halimzuii mlalamikaji kufuata njia sahihi ya madai.
