Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kuanza kwa mchakato mpana wa mapitio ya kanuni, sheria, na ada za leseni zinazosimamia vyombo vya habari vya mtandaoni. Hatua hiyo ni mwitikio wa moja kwa moja kwa malalamiko ya muda mrefu ya wadau wa habari nchini ambao wamekuwa wakidai kuwa mfumo wa sasa unakandamiza ubunifu na unaua ajira kwa vijana.
Akizungumza katika kikao kazi kizito kilichowakutanisha viongozi wa Serikali , mabloga na waandishi wa habari mtandaoni, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Kuwe Bakari, alisema Serikali imekubali “kusikia kilio” hicho.
Dkt. Bakari alibainisha kuwa kikwazo kikubwa kimekuwa ni gharama kubwa za leseni na urasimu wa kikanuni ambao umekuwa ukiwafanya waandishi wengi kushindwa kurasimisha kazi zao. Ili kuhakikisha suluhu ya kudumu inapatikana, amewaelekeza wadau kupitia TBN na JUMIKITA kuteua wajumbe wanne watakaoungana na jopo la wataalamu wa TCRA kuandaa mapendekezo ya mabadiliko ya ada na sheria.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, aliwasilisha uchambuzi wa kina unaoonyesha jinsi Tanzania ilivyokuwa na vizingiti virefu ikilinganishwa na nchi za Afrika Mashariki.
Msimbe alieleza kuwa wakati mwanablogu wa Tanzania analazimika kulipia zaidi ya shilingi 500,000 hadi 1,000,000 kama ada ya maombi na leseni, nchini Kenya hakuna hitaji la leseni ya gharama hiyo, na nchini Uganda ada ni rafiki (Tsh 60,000 – 100,000).
Alisisitiza kuwa mfumo wa sasa unamfanya mwanablogu wa Kitanzania kutumia mtaji wake kulipia ‘karatasi’ za Serikali badala ya kununua vifaa bora kama kamera na maikrofoni, jambo linalopunguza uwezo wa kushindana kimataifa.
Pamoja TCRA kuzungumzia suala la ada na leseni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amebainisha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuachana na mfumo wa kutumia adhabu dhidi ya wanahabari wa mtandaoni na badala yake kuanza kuwalea kupitia uwezeshaji wa kiuchumi.
Msigwa katika kikao hicho pia alitangaza kuwa Serikali inakusudia kuwa na mfuko unaolenga kuwawezesha wanablogu na waandishi wa mtandaoni kumudu kumiliki vitendea kazi vya kisasa na kukuza taaluma yao.
Msigwa alifafanua kuwa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha waandishi wa mitandaoni na mabloga ambao wengi waio ni Gen Z wanatambuliwa kama washirika muhimu wa maendeleo, na si watu wa kuandamwa na faini pekee.
Aidha, katika kukabiliana na changamoto za kodi zinazowakabili mabloga, Msigwa aliahidi kuwa Serikali itakutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kutatua kero za kodi kubwa ambazo hazilingani na kipato cha waandishi. Alisema kuwa lengo ni kuhakikisha blogu zinatambuliwa kama biashara ndogo (SMEs) zinazochangia pato la taifa kupitia utalii na uwekezaji, badala ya kuzitazama kama vyombo vikubwa vya habari vyenye uwezo mkubwa wa kifedha.