KIKOSI cha Coastal Union kinatarajia kurudi kambini Desemba 27 mwaka huu tayari kwa ajili ya kujiweka fiti na michezo iliyo mbele yake huku kocha mkuu wa timu hiyo, Mohammed Muya akiweka wazi kuwa ametoa program maalum kwa nyota wake kabla ya kurudi siku hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Muya amesema amefanya hivyo kwa kutoa programu kwa wachezaji wake kwa lengo la kuona timu inarejea ikiwa katika ubora na sio kuanza moja kutokana na mapumziko ya muda mrefu kupisha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 inayoanza Jumapili.
“Nimetoa program kwa wachezaji wangu wiki moja kabla ya kurudi kambini kuendelea na maandalizi ya msimu. Hatupo vizuri sana hatutaki kuanza moja na ligi imetoa picha ya ushindani ulivyo hivyo kutokana na hilo nimewapa mpango wachezaji nini wakifanye wakiwa majumbani kwao, a;isema na kuongeza:
“Levo ya utimamu wa mwili kwa wachezaji tutakaporudi ndio itakayotoa picha ni nani alikuwa anazingatia kile alichopewa akiwa nje ya timu na tumepanga ratiba ya kurudi mapema ili kutoa nafasi kwa uongozi kufanya uamuzi wa kuachana na nyota ambao watatoka kupisha sajili nyingine za dirisha dogo lijalo.”
Akizungumzia kuhusu kikao cha usajili wa dirisha dogo, Muya amesema mambo yaliingiliana viongozi walishindwa kukutana naye ndio sababu ya kurudisha timu mapema kambini kabla ya kufanya uamuzi wa kupunguza na kuongeza idadi ya wachezaji.
“Kikao hatujafanikiwa kukaa kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu, lakini viongozi wameahidi kufanya hivyo mapema kabla ya dirisha kufunguliwa ili kutoa mwanya kwa wachezaji ambao watatolewa kwa mkopo hata wale ambao wataachwa kupata nafasi ya kusajiliwa na timu nyingine.”
