Sh11.3 bilioni kutumika kuwapa utambulisho watoto

Dar es Salaam. Serikali inafanya maandalizi ya usajili wa watoto wenye umri chini ya miaka 18 ili kutoa namba ya kipekee ya utambulisho watakayoipata pindi wanapozaliwa hadi mwisho wa maisha yao.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawe katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo Ijumaa Desemba 19, 2025 alipofanya ziara ya ukaguzi wa uzalishaji wa vitambulisho katika kituo cha kuchakata taarifa cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Kwa mujibu wa Simbachawene, Sh11.3 bilioni zimetengwa kwa ajili ya mchakato, huku wilaya za Kilolo, Kusini Unguja na Rungwe zitatumika mfano wa majaribio, akiwakumbusha wananchi waliojiandikisha kuchukua vitambulisho vyao.

Waziri Simbachawene amefafanua kuwa namba hiyo itakayotambua watoto ndio jambo lililopo mbeleni na litaondoa malalamiko kwa sababu mtu atakuwa anatambulika pindi anapozaliwa.

Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene akioneshwa taarifa za muombaji wa kitambulisho na Meneja Uhakiki na Usambazaji Vitambulisho, Emmanuel Joshua wakati wa ziara katika Kituo cha Kuchakata Taarifa cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Hata hivyo, katika taarifa hiyo kwa umma haikueleza kwa kina mchakato huo utaanza lini.

Katika hatua nyingine, Simbachwene amesema kuna vitambulisho vilivyozalishwa lakini wahusika hawajafika kuvichukua,  hivyo, amewataka kufika vituo au ofisi za wilaya walizojiandikishia kuvichukua, akisema ukomo wa matumizi ya utambulisho (NIN) ni miaka mitatu.

“Watu wafike katika maeneo waliyojiandikisha kuchukua kitambulisho ambacho hivi sasa kimeunganishwa na kadi ya bima ya afya, leseni ya udereva na mifuko ya hifadhi ya jamii. Hatua hii imemrahisishia mwananchi pindi anapotaka kupata huduma za kiafya au mfuko wa jamii,” ameeleza Simbachawene.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Omar Mmanga amesema mamlaka inaendelea na utambuzi na usajili wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora) ambapo watu 465 wametambuliwa na kuandikishwa hadi sasa.

“Lengo ni kuwafikia Watanzania ili kuwa na vitambulisho popote walipo, hadi sasa jumla ya vitambulisho 21,245,975 vimezalishwa nchini,” amesema Mmanga.