Mlandege, Singida BS kufungua dimba Mapinduzi Cup 2026

RATIBA ya Kombe la Mapinduzi 2026 imewekwa hadharani ikionyesha Mlandege na Singida Black Stars zitafungua dimba la michuano hiyo Desemba 28, 2025.

Kwa mujibu wa Katibu wa Kamati ya Kombe la Mapinduzi 2026, Rashid Said Suleiman, mechi hiyo itaanza saa 10:15 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, ikifuatiwa na Azam dhidi ya URA, saa 2:15 usiku uwanjani hapo.

Suleiman amesema hatua hiyo ya makundi na nusu fainali, mechi zote zitachezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, kisha fainali imepangwa kuchezwa Uwanja wa Gombani uliopo Pemba, Januari 13, 2026.

“Kwa sababu mara ya mwisho kumalizia kwa namna hii ya klabu kabla ya iliyopita kushirikisha timu za taifa, bingwa alikuwa Mlandege, hivyo tunawachukulia kama bingwa mtetezi wa mashindano haya.

“Kwa maana hiyo, yeye ndiye atafungua mashindano yetu kwa siku hiyo kukutana na timu ya Singida.

“Siku hiyohiyo, usiku wake tutakuwa na mechi kati ya Azam na URA,” amesema Suleiman.

Suleiman amesema Desemba 30, 2025 kutakuwa na mapumziko ili kutoa fursa kwa Watanzania kushuhudia Taifa Stars ikicheza mechi ya mwisho hatua ya makundi katika fainali za AFCON 2025 dhidi ya Tunisia huko nchini Morocco. Pia Januari Mosi 2026 yatakuwepo mapumziko ya mwaka mpya.

Katika hatua nyingine, Suleiman amesema baada ya awali kuzitaja timu nane zitakazoshiriki mashindano hayo, wameziongeza mbili ambazo ni TRA United na Mwembe Makumbi.

“Mashindano yetu yatakuwa na timu kumi kutoka nane za mwanzoni ambazo tulizitaja. Tumeziongeza TRA United kutoka Tanzania Bara na Mwembe Makumbi ya hapa Zanzibar.

“Hivyo kutokana na hilo, pia tutakuwa na makundi matatu, kundi moja litakuwana timu nne ambapo mbili zitakazomaljza nafasi za juu zitafuzu nusu fainali, huku makundi mengine yenye timu tatu, vinara ndio watafuzu nusu fainali,” amesema.

Suleiman alizitaja timu hizo kumi zitakazoshiriki ni Simba, Yanga, Azam, Singida Black Stars na TRA United zote kutoka Tanzania Bara, upande wa Zanzibar zitakuwepo Fufuni, Mlandege, KVZ na Mwembe Makumbi wakati URA ikitokea Uganda.

RATIBA
Desemba 28, 2025
Mlandege vs Singida BS (Saa 10:15 jioni)
Azam vs URA (saa 2:15 usiku)

Desemba 29, 2025
Fufuni vs Mwembe Makumbi (Saa 10:15 jioni)
KVZ vs TRA (Saa 2:15 usiku)

Desemba 31, 2025
Mlandege vs URA (Saa 10:15 usiku)
Singida BS vs Azam (Saa 2:15 usiku)

Januari 2, 2026
Azam vs Mlandege (Saa 2:15 usiku)

Januari 3, 2026
Singida BS vs URA (Saa 10:15 jioni)
Simba vs Mwembe Makumbi (Saa 2:15 usiku)

Januari 4, 2026
Yanga vs KVZ (Saa 2:15 usiku)

Januari 5, 2026
Fufuni vs Simba (Saa 2:15 usiku)

Januari 6, 2026
Yanga vs TRA (Saa 2:15 usiku)

Januari 8, 2026
Nusu Fainali ya Kwanza (Saa 2:15 usiku)

Januari 9, 2026
Nusu Fainali ya Pili (Saa 2:15 usiku)

Januari 13, 2026
Fainali (Saa 2:15 usiku)

MAKUNDI
Kundi A: Mlandege, Azam, Singida Black Stars, URA

Kundi B: Simba, Mwembe Makumbi, Fufuni

Kundi C: Yanga, KVZ na TRA