Utalii mpya wa usiku kuvutia watalii Tarangire

Tarangire. Ili kuendelea kuvutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi, utalii wa usiku unatajwa kuwa kivutio kikubwa katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.

Aidha, kivutio kingine kipya ni kutambua tembo wanaozaa pacha, ambapo mchakato wake upo katika hatua za utafiti, hatua inayotarajiwa kuongeza idadi ya watalii na kuchangia kukuza pato la Taifa.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Desemba 19, 2025 na ofisa uhifadhi anayeshughulikia masuala ya utalii katika hifadhi hiyo.

Amesema utalii mpya wa usiku utaongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi, hatua inayotokana na jitihada za Serikali za kutangaza na kuanzisha mazao mapya ya utalii nchini.

Kuhusu tembo wanaozaa pacha, ofisa huyo amesema suala hilo linaendelea katika mchakato wa tafiti mbalimbali ili kuhakikisha taarifa sahihi zinapatikana.

Mmoja ya waongoza watalii kutoka kampuni ya Serengeti African, Luka Pallangyo amesema katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka watalii wengi hupendelea kutembelea hifadhi mbalimbali, baadhi wakiwa na familia zao.

“Wageni wengi wanapenda mazingira na tunapoelekea mvua inanyesha, hivyo kunakuwa na mandhari ya kijani inayovutia zaidi,” amesema.

Mmoja wa watalii hao kutoka Marekani, Kelly Anderson, amesema Tanzania ni nchi yake ya 10 barani Afrika kutembelea na amevutiwa na mandhari katika Hifadhi za Taifa za Serengeti na Tarangire na ukarimu wa Watanzania.

Amesema mwaka huu amekuja kutembelea hifadhi mbalimbali hapa nchini katika kuadhimisha kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa na kuwa anatarajia kurudi mwakani tena kutembelea vivutio vingine.

“Kiukweli kwa namna nimeona hifadhi hizo, nimeona wanyama na mandhari ya kuvutia nzuri zaidi ya inavyoonekana kwenye picha. Kuna uzuri wa asili na nimejihisi kama niko nyumbani nikiwa hapa Tanzania,” amesema na kuongeza;

“Tanzania ni nchi ya 10 Afrika na nina tamani kutembelea nchi zote 54 za Afrika ila kabla sijaendelea na nchi zingine lazima nirudi Tanzania mwakani, kwani ninajiona niko nyumbani,” amesema.

Naye Janine Hellwig kutoka Ujerumani, amesema katika Hifadhi za Taifa za Ziwa Manyara na Tarangire ambazo wametembelea, wamejionea wanyama wa aina mbalimbali.

“Tumefurahi sana kwani tumeona wanyama wengi wakiwemo chui, tembo, twiga, viboko, nyati na wengine, tunaamini tunapoendelea kwenye hifadhi nyingine tutajionea wanyama wengine zaidi na vivutio vingine vilivyopo Tanzania,” amesema.