Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha Disemba 19, 2025
Simbachawene alitoa kauli hiyo Disemba 18, 2025, alipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani katika ziara yake ya kikazi ya kukagua uzalishaji wa vitambulisho vya Taifa katika Kituo cha Kuchakata Taarifa cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
“Mara nyingi wageni wamekuwa wa kwanza kuona na kutumia fursa za kiuchumi kuliko wananchi wa asili, ni muhimu hata wazawa wakafaidika na maendeleo yanayopatikana,” alibainisha Simbachawene.
Akizungumzia vitambulisho vya Taifa, Waziri huyo alieleza, vitambulisho vya NIDA vina manufaa makubwa ikilinganishwa na vitambulisho vya kawaida, kwani kwa sasa vimeunganishwa na huduma nyingine muhimu.
Alieleza kuwa ,vitambulisho hivyo sasa vinaunganishwa na kadi ya Bima ya Afya, leseni ya udereva pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.
Vilevile Simbachawene alifafanua, Serikali inaendelea na uzalishaji wa vitambulisho hivyo, akibainisha kuwa changamoto ndogo zilizokuwepo zinaendelea kushughulikiwa, huku akiahidi kuwa ifikapo Februari 2026 lengo la kuwafikia Watanzania milioni 31 litakuwa limefikiwa.
“Kwa sasa tumefikia Watanzania milioni 22, tukiwa na upungufu wa takribani milioni 9, tayari zoezi la utambuzi limeanza na baada ya hatua hii tutapiga hatua kubwa zaidi,” aliongeza Simbachawene.
Hata hivyo, Waziri huyo alisema Serikali inaangalia uwezekano wa kufanya marekebisho ya sheria ya NIDA ili kuruhusu zoezi la utambuzi kuanza kwa watoto kuanzia vichanga hadi umri wa miaka 18, hatua itakayowezesha mtoto kutambulika rasmi tangu anapozaliwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alipokea maelekezo yaliyotolewa na Waziri na kumshukuru kwa ziara na mwongozo alioutoa katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
.jpeg)
