Katambi aitaka NDC kuleta mapinduzi ya viwanda

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi ameliagiza Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kuchukua hatua madhubuti za kuleta mapinduzi ya viwanda nchini kwa kufungua viwanda vingi zaidi na kuzalisha fursa za ajira, hususan kwa vijana.

Aidha, amelitaka shirika hilo kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yake na kuimarisha uwajibikaji ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta ya viwanda na kukuza uchumi wa Taifa.

Katambi ametoa kauli hiyo jana Desemba 18, 2025 jioni alipofanya ziara ya kikazi katika makao makuu ya NDC.

Amesisitiza umuhimu wa shirika hilo kusimamia kwa umakini maeneo yote yaliyo chini ya dhamana yake, huku likifanya kazi kwa kasi, weledi na ufanisi wa hali ya juu.

Amesema Serikali imejipanga kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya viwanda, ikiwamo kuwezesha upatikanaji wa mitaji, kutoa ushauri wa kibiashara na kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kwa lengo la kupanua wigo wa ajira na kuinua ustawi wa wananchi, hasa vijana.

Amefafanua kuwa mkakati wa Serikali ni kuleta mageuzi makubwa ya viwanda kuanzia viwanda vidogo, vya kati hadi vikubwa, ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa na kuongeza thamani ya rasilimali za ndani.

“NDC ihakikishe inalenga kuanzisha viwanda vidogo sana, vidogo, vya kati na vikubwa, sambamba na kufufua kwa haraka viwanda vilivyodorora, ili kuongeza uzalishaji na idadi ya viwanda nchini,” amesema Katambi.

Aidha, amehimiza mshikamano, mashauriano ya mara kwa mara na kuondoa urasimu usio wa lazima ndani ya shirika, akisisitiza kuwa NDC inapaswa kuwa kiungo kati ya Serikali na wananchi badala ya kuwa kikwazo.

Ameongeza kuwa mafanikio ya kiuchumi ya nchi yoyote yanategemea uwepo wa viwanda imara vinavyoweza kuzalisha ajira na kuongeza thamani ya rasilimali zake.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NDC, Valentine Simkoko amesema shirika hilo linasimamia  miradi  mbalimbali ya kimkakati na  linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi.

Ameitaja baadhi ya miradi inayosimamiwa na NDC kuwa ni Mchuchuma na Liganga, Magadi Soda ya Engareka, pamoja na tathmini ya mali za wananchi wanaohusika katika miradi ya makaa ya mawe Katewaka na chuma ghafi cha Maganga Matitu.

Simkoko ameongeza  NDC pia imeingia mikataba ya ubia na wawekezaji katika mradi wa chuma wa Maganga Matitu, pamoja na kusaini mkataba na Kampuni ya Labiofam S.A. kwa ajili ya kuhamisha teknolojia ya uzalishaji wa mbolea hai nchini.