Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa wenye thamani ya Sh280 bilioni ni mojawapo ya mradi utakaojibu majibu ya kero zinazowakabili Watanzania ikiwamo ya umasikini.
Pia, Dk Mwigulu amesema mradi huo ni miongoni mwa maeneo yanayofafanua kauli na ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kuendeleza miradi iliyoachwa na mtangulizi wake (Hayati John Magufuli).
Ameeleza hayo Ijumaa Desemba 19, 2025 akikagua ujenzi wa bandari ya uvuvi inayojengwa Kilwa Masoko mkoani Lindi, katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi aliyoanzia mikoa ya Songwe na Mbeya.
Dk Mwigulu amesema pamoja na Tanzania kubarikiwa rasilimali ikiwamo ya bahari, lakini huwezi kwenda na kutumia mashua kuvua samaki kwenye maji marefu au meli kubwa haziwezi kuja kuvua nchini.
Kutokana na hilo, Dk Mwigulu amesema ndio maana Serikali kwa kutumia fedha za ndani iliamua kujenga bandari ya uvuvi ya kisasa, kama zilizopo katika mataifa mbalimbali ya Ulaya.
“Mradi huu unakwenda kutengeneza ajira, kuongeza kipato cha Watanzania wanaojishughulisha na sekta ya uvuvi. Hii ndio maana hali ya uongozi unaocha alama.
“Hii (bandari) ni mali ya Watanzania, inakwenda kuwapa kipato na kubadilisha maisha ya Watanzania, inakwenda kuongeza kipato cha Watanzania,” ameeleza Dk Mwigulu.
Dk Mwigulu amesema mradi huo uliofikia asilimia zaidi ya 90 ukikamilika unakwenda kutengeneza ajira zaidi ya 30,000, akisema hivyo ndivyo changamoto za Watanzania zinavyopaswa kutatuliwa.
“Hili linatoa jawabu la kupunguza umasikini na linatoa jawabu la kuongeza kipato. Safari iliyoandikwa kwenye Dira ya 2050 inaanza na miradi mikubwa ukiwamo huu ambao haujawahi kushuhudiwa ndani ya nchi,” amesema Dk Mwigulu.
Mtendaji mkuu huyo wa Serikali, amesisitiza kuwa mradi huo unakwenda kutatua tatizo la ajira lililopo kwa vijana na kina mama katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Bashiru Ally amesema bandari hiyo ina viwango vya kisasa na wameanza mchakato wa kuithibitisha kimataifa katika viwango vya kikanda na kimataifa.
“Bandari hii inaelekea kukamilika tunatarajia kupata ajira za kutosha kutokana na mradi huu. Huu utakuwa ukanda wa viwanda, kampuni yetu ya uvuvi imeanza mchakato wa kujenga kiwanda cha kuchakata Samaki,” amesema Dk Bashiru.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amesema kumekuwa na ushirikiano mkubwa kati ya Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM), katika kuhakikisha mradi wa ujenzi wa bandari hiyo unatekelezwa kwa ufanisi.
Msimamizi wa ujenzi wa bandari hiyo, George Kwandu amesema eneo linalotekelezwa mradi lina ekari 48 likijumuisha ujenzi huo, sambamba na viwanda ambavyo ni fungamanishi na mradi huo.
Amesema wavuvi wakimaliza kuvua Samaki, watakwenda katika bandari hiyo na kushusha katika gati lenye urefu wa mita 315, lenye uwezo wa kuegesha meli 10 za uvuvi za mita 30 kushusha katika eneo hilo kwa wakati mmoja.
Mbunge wa Kilwa Kusini (CCM)Hasnain Dewji amesema mradi huo utawezesha maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Kilwa, huku akikumbushia ahadi ya Rais Samia kuhusu fidia ya wananchi 470 waliopisha ujenzi wa Kilwa Masoko.
“Kuna changamoto hapa Kilwa Masoko, kuna wananchi 470 hawajalipwa fidia zao kwenye mradi wa uwanja wa ndege, jambo hili unalifahamu tangu ukiwa Waziri wa Fedha, tunakuomba useme neno,” amesema Dewji.
Hata hivyo, Dk Mwigulu ameahidi kulichukua kwa ajili ya kufanyiwa kazi, huku akimtaka mbunge huyo, kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa kila kilichoahidiwa na Rais Samia kitatekelezwa ingawa kwa awamu.
