Dijitali yatajwa kiungo muhimu ujumuishi wa kifedha

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga amesema matumizi ya teknolojia ya kidijitali na huduma za kifedha kwa njia ya simu ni chombo muhimu katika kuwezesha wanawake na vijana katika kuhakikisha maendeleo binafsi na ya Taifa.

Ukuaji wa teknolojia ni miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa kwa kirefu na leo Ijumaa Desemba 19, 2025 na wadau kutoka taasisi mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya maendeleo ya kiuchumi na kifedha nchini, katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 20 ya Shirikisho la Wafanyabiashara wanawake Tanzania, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Kapinga ametilia mkazo uwezeshaji wa wanawake na vijana akisema ni jambo muhimu katika kuhakikisha maendeleo jumuishi nchini.

“Serikali inatambua umuhimu na itaendelea kuwezesha wanawake na vijana kiuchumi, ikitazamia kuona wajasiriamali chipukizi, vijana na wanawake, wanafikia mafanikio makubwa kwa maendeleo ya uchumi wa nchi,” amesema.

Ameipongeza TWCC kwa kuyafikia na kuwawezesha makundi hayo nchini, kwa kuhakikisha wanawake na vijana wanawezeshwa kufikia mafanikio ya kiuchumi kupitia biashara zao.

Waziri Kapinga amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono na kusaidia wadau wote wanaowekeza katika miradi ya vijana na wanawake nchini ili kuhakikisha kundi hilo linanufaika na fursa za kiuchumi nchini.

Waziri wa Viwanda na Biashara (katikati), Judith Kapinga, na viongozi wa Taasisi mbalimbali, akikata keki katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Miaka 20 ya Shirikisho la Wafanyabiashara wanawake Tanzania (TWCC) jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa Desemba 19, 2025.

Alichokisema Kapinga kimeungwa mkono na Mkurugenzi wa Kituo cha Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi nchini (NEEC) , Beng’i Issa, akitaja matumizi ya simu za mkononi kama chachu ya kuwezesha na kuongeza ujumuishi wa kifedha.

“Kwa utafiti wa mwaka juzi, pengo la kifedha kati ya wanawake na wanaume limepungua kutoka asilimia 10 hadi asilimia 5; matumizi ya simu za mkononi yamechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ujumuishi wa kifedha,” amesema Beng’i Issa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ujumuishi wa Kifedha nchini.

Hata hivyo, amebainisha kuwa bado wanawake wanaomiliki akaunti za benki ni wachache ikilinganishwa na wanaume, akitoa wito wa kufanyika tathmini ili kujua vikwazo na suluhu.

“Baadhi ya changamoto ni kwamba wanawake wengi hasa waliopo vijijini wanatumia simu za viswaswadu, hivyo hawana uwezo wa kuingia kwenye mifumo ya kimtandao yenye fursa za kibiashara. Wengine hawana biashara rasmi zinazowaingiza katika mifumo ya mzunguko rasmi wa fedha.

“Kwa utafiti wa IFC hivi karibuni umeonesha ni asilimia 12 tu ya wanawake wana akaunti za benki,” amesema akitoa wito kwa wanawake kurasimisha biashara zao na kuingia katika mifumo rasmi ya ujumuishi wa kifedha.

Kwa upande wake, Rais wa TWCC, CPA Mercy Sila, ametoa wito kwa wadau kuunganisha nguvu katika kuwaunganisha na kuwawezesha wafanyabiashara nchini ili waweze kukua kiuchumi.

“Mafanikio mengi yamefikiwa, lakini nitoe wito kwa wadau wote tuunganishe nguvu katika kuwaunganisha na kuwarasimisha wanawake na vijana ili wawe na biashara endelevu,” amesema.

Akifafanua mafanikio ya taasisi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Dk Mwajuma Hamza, amesema miaka 20 ya taasisi hiyo imekuwa na mafanikio makubwa katika kuwezesha wanawake.

Amesema pamoja na mafanikio yake, taasisi hiyo inalenga kuzunguka nchini kote kuona mafanikio na changamoto wanazopitia wanawake na vijana kiuchumi ili kuweza kuwasaidia kufikia malengo yao.

Wadau mbalimbali wakishiriki Maadhimisho ya miaka 20 ya Shirikisho la Wafanyabiashara wanawake Tanzania (TWCC) jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa Desemba 19, 2025.

“TWCC kwa miaka 20, imewafikia wanawake na vijana wengi sana nchi nzima ambao wamejengewa uwezo na kurathimishwa biashara zao, hatua iliyowawezesha kuingia katika ujumuishi wa  kifedha na kuinua hali ya maisha yao,” amesema.

Akitilia mkazo wa kufungua fursa za kikanda, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa taasisi ya Trade Mark Africa, Dk Monica Hangi ametoa wito wa kuchangamkia fursa za kimataifa, akiwataka wanawake wa Tanzania kuchangamkia fursa za kiuchumi Afrika Mashariki na katika masoko mengine ya kikanda.

“Kwa sasa dunia imefunguka, zipo fursa nyingi katika masoko ya kimataifa likiwemo soko la Afrika Mashariki, changamkieni fursa hizo,” amesema.