Mafunzo ya urubani nchini yapunguza gharama kwa Watanzania

Dar es Salaam. Tangu kuanzishwa kwa kozi ya urubani katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), kumewesha mafunzo hayo kupunguza gharama kwa Watanzania wenye ndoto ya kuendesha ndege.

Gharama ya mafunzo ya urubani kwa NIT tangu yaanzishwe Julai 2025 kwa daraja la awali (PPL) mafunzo ya nadharia ni Sh5,550,000 mafunzo ya vitendo (kuendesha ndege) kwa  kwa saa moja ni Sh648,000 ambapo muda wa chini wa mafunzo ya vitendo ni saa 45 ili kumuwezesha mwanafunzi kuhitimu. Jumla ya gharama kwa saa zote 45 ni Sh29.1 milioni.

Gharama hizo za NIT ikilinganishwa na gharama za nje ya nchi ambazo ni za chini ni takriban Sh50 milioni (lakini inategemea na nchi au chuo kinachotoa mafunzo hayo).

Akizungumza leo, Desemba 19, 2025, katika mahafali ya 41 ya NIT yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Mkuu wa chuo hicho, Profesa Prosper Mgaya, amesema tangu kuanza rasmi kwa mafunzo ya urubani Julai 2025, tayari wanafunzi 20 wamejiunga.

Mgaya ameeleza kuwa kati ya hao, 10 tayari wamemaliza mafunzo ya awali (ground school), huku saba kati yao wakiwa tayari wanaweza kurusha ndege angani bila usimamizi.

Aidha, amebainisha kuwa chuo kimeendelea kutoa mafunzo katika taaluma nyingine za usafiri wa anga, ikiwamo wahudumu wa ndege na wataalamu wa ukarabati wa ndege.

Wahitimu wa fani mbalimbali kutoka Chuo cha Taifa cha  Usafirishaji (NIT) wakishangilia katika mahafali ya 41 ya chuo hicho yaliyofanyika leo Disemba 19, 2025 jijini Dar es Salaam.

Mgaya amefafanua kuwa yote haya yamewezekana kutokana na Serikali kuwekeza takribani Sh57 bilioni katika Kituo cha Umahiri cha Usafiri wa Anga, hatua iliyowezesha kuboresha mafunzo na kuongeza idadi ya wataalam wazawa.

 “Kwa muda mrefu Taifa letu limekuwa likitegemea mafunzo ya wataalamu wa usafiri wa anga kutoka nje ya nchi, Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kusomesha wataalamu kutoka nje ya nchi kuanzishwa kwa mafunzo hayo kutasaidia kupunguza gharama hiyo iliyokuwa ikitumika,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amekipongeza chuo hicho kwa kuendelea kupanua wigo wa mafunzo katika sekta ya uchukuzi, hatua inayosaidia kuongeza idadi ya wataalamu, hususan katika usafirishaji wa anga, kwa kuanza rasmi kutoa mafunzo ya urubani.

Amesema jitihada hiyo itasaidia kupunguza gharama kubwa ambazo Serikali na Watanzania walikuwa wakiitumia kupata mafunzo hayo nje ya nchi.

Aidha, kuanzishwa kwa mafunzo haya ndani ya nchi kutaongeza idadi ya wataalamu wazawa katika taaluma ya uhandisi, huku wakiimarisha sekta ya uchukuzi nchini.

”Kuanza kwa kozi hizo kutatoa fursa kwa Watanzania kupata masomo haya adhimu hapa nchini kwa gharama nafuu na hivyo kuwezesha sekta  ya usafiri wa anga kupata watalaamu stahiki ambao wataiendesha kwa ufanisi,” amesema.

Ameeleza kuwa hatua hiyo itachochea ukuaji wa sekta nyingine kama vile utalii, biashara na kilimo, huku ikichangia pia katika kuimarisha uchumi wa Taifa kwa jumla.

Mbarawa ameongeza kuwa Serikali, ikitambua umuhimu wa kuwa na wataalamu wa kutosha katika fani hiyo, imechukua hatua ya kuongeza ndege tatu mpya kwa ajili ya mafunzo ya urubani.

Pia, Mbarawa amesema Serikali ipo katika hatua ya kuandaa mapendekezo ya kutunga sheria ya bodi ya wataalamu wa uchukuzi.

Amesema mapendekezo ya sheria  yameandaliwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji, baada ya kutambua uhitaji wa kuwepo kwa bodi hiyo.

Lengo kuu la kuanzishwa kwa bodi hiyo, amesema ni kutambua, kusajili na kusimamia weledi pamoja na maadili yanayoweza kuongoza wataalamu wa uchukuzi na usafirishaji nchini.

 “Bodi hiyo itahakikisha kazi zote za usafirishaji na uchukuzi zinasimamiwa na watu wenye taaluma katika eneo hilo,” amesema.