Dar es Saalam. Kadri matumizi ya mitandao ya kijamii yanavyozidi kuongezeka, ndivyo changamoto mpya za kidijitali zinavyoibuka, ikiwemo matumizi ya akaunti bandia maarufu kama bots, ambazo zimeanza kutawala mijadala mingi, kwa lengo la kushawishi au kupotosha maoni ya umma.
Ingawa suala la bots si geni duniani, nchini Tanzania tatizo hilo limeshika kasi kwa sasa, hasa kuanzia kipindi cha Uchaguzi Mkuu, ambapo mijadala mitandaoni ilijaa hashtag kama #OktobaTunatiki na #NoReformsNoElection.
Bots hutengenezwa mahsusi kusambaza ujumbe fulani mara nyingi, ili kuunda taswira ya uungwaji mkono mpana, hali inayoweza kuwapotosha watumiaji wa mitandao hiyo.
Baada ya matukio ya vurugu ya Oktoba 29 bots zilirejea tena kwa kasi, safari hii zilikuwa zikisukuma ujumbe za upande mmoja, ili ionekane kama kila mtu anakubaliana nao.
Hali hiyo hutengeneza dhana ya uongo kwamba jamii nzima inakubaliana na msimamo fulani, ilhali kwa uhalisia ni kazi ya programu zinazoendeshwa na roboti kwa malengo maalumu.
Athari za matumizi ya bots ni pana, zikiwemo kupotosha mjadala wa umma, kueneza taarifa zisizo sahihi pamoja na taarifa za uongo zinazotolewa kwa makusudi sambamba na kuchochea migawanyiko au taharuki katika jamii.
Akaunti nyingi za bot huonekana kwa kuangalia kwa makini taarifa za ‘profaili’ za wahusika. Mara nyingi hutumia majina yasiyo na utambulisho binafsi mfano John Smith2024 au Africa Voice, bila picha halisi ya mtu, bali hutumia picha za jumla zilizopakuliwa mtandaoni.
Akaunti hizo pia huwa na wafuasi wachache au hufuata akaunti nyingine nyingi zinazofanana kimuundo na kimaudhui, hali inayoashiria ni mtandao wa akaunti bandia unaoendeshwa kwa lengo moja mahsusi.
Mbali na profaili, mienendo ya akaunti hizo huibua mashaka, ikiwemo kuchapisha ujumbe mara kwa mara ndani ya muda mfupi bila kupumzika, mara nyingi kwa kutumia maneno yale yale kwenye mijadala tofauti.
Aidha, lugha wanayotumia huonekana kuwa ya kimitambo, huku majibu yao yakishindwa kujibu hoja halisi iliyoulizwa, na wakati mwingine hujibu kwa kasi isiyo ya kawaida hata kama ni usiku wa manane.
Viashiria hivi vinavyoweza kuwasaidia watumiaji wa mitandao ya kijamii kutofautisha kati ya akaunti halisi na bots.
