Baada ya Steve Barker kutambulishwa Simba, Stellenbosch yatoa tamko

KLABU ya Stellenbosch kutoka Afrika Kusini, imetoa tamko ikithibitisha kuwa, Steve Barker amejiuzulu nafasi yake ya Kocha Mkuu ili kuchukua jukumu jipya la kuinoa Simba SC ya Tanzania.

Hiyo imekuwa siku moja baada ya Simba kumtambulisha raia huyo wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 57 kuchukua nafasi ya Dimitar Pantev ambaye iliachana naye Desemba 2, 2025 kwa makubaliano ya pande mbili.

Barker awali alijiunga na Stellenbosch FC kama kocha msaidizi wa Sammy Troughton katika msimu wa kwanza wa klabu hiyo, kabla ya kuteuliwa kuwa Kocha Mkuu Julai 2017, uteuzi uliosaidia kuiweka Stellenbosch kwenye ramani ya soka la Afrika Kusini.

Chini ya uongozi wake, Barker aliiongoza timu katika mechi 309 kwenye mashindano yote. Aliisaidia Stellenbosch kupanda daraja kwenda Ligi Kuu ya Afrika Kusini baada ya kutwaa ubingwa wa National First Division msimu wa 2018–2019. Pia aliandika historia kwa kuwa timu ya kwanza kushinda masindano mapya ya Carling Knockout mwaka 2023.

Aidha, Barker aliiongoza Stellenbosch kufika fainali za MTN8 kwa misimu miwili mfululizo mwaka 2024 na 2025, pamoja na kufuzu mara mbili mfululizo kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumza kuhusu uamuzi wake wa kuondoka baada ya karibu miaka tisa ndani ya klabu hiyo, Barker amesema: “Ni uamuzi wenye hisia mchanganyiko, lakini ninaamini muda umefika kwa Stellenbosch kuanza enzi mpya chini ya uongozi mwingine. Naomba klabu iendelee kupata mafanikio siku zijazo.”

“Ninaamini kuchukua changamoto mpya na ya kusisimua katika moja ya klabu kubwa barani Afrika, ni hatua muhimu kwa maendeleo yangu binafsi na malengo yangu kama kocha. Nashukuru kuwa muda wangu Stellenbosch imefungua mlango huo.

“Ningependa kuwashukuru watu wote ndani ya klabu kwa mchango wao mkubwa katika safari yangu hapa Stellenbosch. Nitathamini milele kumbukumbu tulizotengeneza pamoja.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Stellenbosch FC, Rob Benadie, alimpongeza Barker kwa mchango wake mkubwa akisema: “Mafanikio ya Steve uwanjani yanaonekana wazi, lakini mchango wake katika kujenga utamaduni, utambulisho na viwango vya kitaaluma vya Stellenbosch FC umekuwa wa muhimu sana.

“Kutumikia klabu moja kwa karibu miaka tisa katika soka la kisasa ni ishara ya uaminifu wa kipekee na kujitolea kwa maono ya muda mrefu ya klabu ingawa kuondoka kwake kunafunga sura muhimu katika historia yetu, klabu ipo katika nafasi nzuri ya kuendelea mbele kwa uthabiti.”

“Kwa niaba ya Stellenbosch FC, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Steve na familia yake kwa kujitoa kwao. Tunawatakia kila la kheri nchini Tanzania.”