Dar es Salaam/Lindi. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema ujenzi wa kampasi ya kilimo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mkoani Lindi utasaidia kuzalisha watafiti na wataalamu wabobezi katika sekta ya kilimo.
Amesema ujenzi huo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha elimu ya juu inakuwa chombo cha mageuzi ya kiuchumi na kijamii.
Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo leo, Jumamosi Desemba 20, 2025, wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kampasi hiyo katika eneo la Ngongo mkoani Lindi, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
“Kupitia kampasi hii, Serikali inalenga kuandaa wataalamu wabobezi wa kilimo, utafiti na biashara ya kilimo watakaosaidia kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao, ajira kwa vijana pamoja na mapato ya wakulima,” amesema.
Ameongeza kuwa kampasi hiyo itaifanya Lindi kuwa lango muhimu la kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika sekta za kilimo, teknolojia, biashara na utafiti.
Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amesema eneo lililotengwa kwa ajili ya kampasi hiyo ni kubwa na lina mipango ya muda mrefu, hivyo amewataka wataalamu wa ardhi na mipango kuhakikisha linalindwa dhidi ya uvamizi.
“Eneo hili lina mipango ya muda mrefu hadi mwaka 2045. Tukifika huko, asiwepo mtu akaanza kuvamia na kuleta shida. Mkoa na wizara tuangalie uwezekano wa kuweka miundombinu itakayolitenga ili lionekane wazi kuwa ni eneo maalumu kwa miaka 20 ijayo,” amesema.
Amesema uwepo wa Naibu Waziri wa Ardhi, Kaspar Mmuya, utumike kutoa maelekezo kwa maofisa ardhi ili wasiotoe hati katika eneo hilo.
“Wasijaribu kumpa mtu hati katika eneo hili. Naliweka akiba. Tutazungumza nikija Wizara ya Ardhi,” amesema.
Dk Mwigulu amesisitiza kuwa wataalamu wa ardhi wanapaswa kuliweka eneo hilo kwenye kumbukumbu zao, ili kuepusha mtu yeyote kutoa hati katika eneo lililotengwa kwa ajili ya kampasi ya chuo.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kupitia mradi wa mageuzi ya elimu ya juu, kampasi 47 zinajengwa, zikiwemo maabara na karakana 309, mabweni 26, ofisi, maktaba na zahanati zaidi ya 1,000 ili kuwezesha shughuli za elimu ya juu.
Amesema ujenzi huo unafanyika katika mikoa mbalimbali na kazi kubwa iliyopo ni kuhakikisha mara tu ujenzi utakapokamilika, shughuli za ufundishaji zinaanza kwa kasi bila kuathiri ubora wa elimu.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jakaya Kikwete amesema kampasi hiyo itakuwa kituo cha kisasa cha maendeleo ya kilimo na tafiti.
“Ni dhamira ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kujenga kampasi hii kuwa taasisi yenye ufanisi wa hali ya juu katika elimu na mafunzo, utafiti na ubunifu kwenye eneo la kilimo. Matumaini yetu ni kwamba siku moja dunia itatambua kuwa kuna kituo mahiri hapa Lindi,” amesema Kikwete, ambaye ni Rais mstaafu wa awamu ya nne.
Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa William Anangisye amesema uwekezaji unaofanyika mkoani Lindi ni sehemu ya utekelezaji wa dhima ya chuo hicho ya kuzalisha maarifa yenye mchango wa moja kwa moja katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia.
Amesema dhima hiyo inatekelezwa kupitia mpango mkakati wa chuo unaolenga kuboresha mifumo ya ufundishaji, ujifunzaji, utafiti na ubunifu kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wanafunzi na watumishi.
Ameeleza kuwa utekelezaji huo unaenda sambamba na mradi wa mageuzi ya elimu ya juu unaotekelezwa na Serikali kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, unaolenga kuboresha mitaala na mazingira ya elimu ili yaendane na mahitaji ya soko la ajira.