Dar es Salaam. Utafiti mpya umebaini kuwa kuzingatia tabia chanya nne za maisha, kunaweza kufanya ubongo kubaki mchanga na wenye afya kwa kipindi cha hadi miaka minane.
Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Florida waligundua kuwa na matumaini mema, kupata usingizi wa kutosha, kudhibiti msongo wa mawazo na kuwa na msaada imara wa kijamii, kulionyesha kuwa na ubongo unaoonekana mchanga zaidi katika vipimo vya uchunguzi.
Tabia hizi huufanya ubongo kuwa wenye afya, utendaji bora zaidi na wenye kupungua kwa viashiria vya kuzeeka kibaolojia.
Mtaalamu na mkufunzi wa saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Muhimbili (Muhas), Faithness Kiondo amezichambua tabia hizo nne kuwa nguzo muhimu za afya ya akili na ubongo kwa ujumla.
Amesema kuwa na matumaini mema husaidia mtu kukabiliana vyema na changamoto za maisha na kupunguza athari hasi za msongo wa mawazo.
Vivyo hivyo katika kupata usingizi wa kutosha ni msingi wa urejeshaji wa kazi za ubongo, ikiwemo kumbukumbu, umakini na udhibiti wa hisia.
“Kudhibiti msongo wa mawazo huzuia athari za muda mrefu zinazoweza kuharibu afya ya akili na mwili. Aidha, kuwa na msaada imara wa kijamii huongeza ustahimilivu wa kisaikolojia na huchangia ustawi wa kihisia na kiakili,” amesema.
Kiondo ameongeza kuwa kwa pamoja, tabia hizi husaidia kudumisha afya bora ya ubongo na kupunguza hatari ya kuzeeka mapema kibaiolojia.
Daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Japhet Swai amesema tafiti hizo si za kwanza kuthibitisha hilo, ingawa zinatofautiana malengo.
Amesema tafiti nyingi zenye msingi wa taaluma mbali mbali zimethibitisha ukweli huu pia kwamba, kuwa na matumaini katika maisha, kupata usingizi mzito wa kutosha, kukabiliana na msongo kila siku na kuwa na jamii unayoweza kuitegemea; ni muhimu siyo tu kwa kuufanya ubongo uwe nyuma ya umri wako bali pia kuongeza umri wa kuishi, kukukinga na magonjwa yasiyoambukiza, kuimarisha uhusiano wa familia na uchumi.
“Matumaini ni muhimu sana katika maisha na kuwa nayo au kutokuwa nayo, hutegemea sana matumizi ya akili ya mtu. Jinsi anavyoyapa maana mambo yanayomtokea maishani, jinsi anavyojiona na jinsi anavyotazama maisha yake ya baadaye,” amefafanua.
Dk Swai amesema hii hutegemea sana malezi ya mtu utotoni, je alilelewa na wazazi waliomfundisha uhalisia wa maisha au alidanganywa?
“Mbili tukumbuke, tunalala usingizi huku tukipitia hatua nne, hatua ya usingizi mzito ndipo ukarabati wa mwili kwa ujumla hufanyika, lakini pia hifadhi ya taarifa kwa ajili ya kukumbuka baadaye hufanyika,” amesema.
Dk Swai amesema ili upitie hatua hiyo, ni lazima ulale si chini ya saa saba mfululizo, uwe umekula chakula chepesi saa mbili hadi tatu kabla ya kulala, ulale chumba chenye giza, ulale chumba chenye ukimya.
“Kumbuka, mfululizo maana yake hakuna simu na ‘washroom’ (kwenda kujisaidia) isizidi mara moja kwa usiku. Usingizi bora na wenye faida ni usingizi wa usiku,” amefafanua.
Dk Swai anafafanua kuwa msongo ni hali ambayo haiepukiki, wasiokabiliwa na msongo ni watu waliokufa tu, msongo wa mawazo ni ishara ya uhai.
Amesema msongo siyo ugonjwa, ni hali inayotokana na jinsi ya kukabiliana na mahitaji ya kila siku ya maisha, hakuna anayeweza kukwepa msongo bali ni kukabiliana nao kwa kufanya mazoezi kila siku.
“Cha kushangaza ni kwamba watu hatuzingatii ingawa wengi tunalijua hili. Msongo wa mawazo ndiyo sababu ya shida nyingi za mtu ikiwemo magonjwa, kukosa maelewano na hali mbaya za kiuchumi,’ amesema.
Utafiti huo uliwafuatilia watu wazima 128 wa umri wa kati na uzee kutoka mabara nne kwa kipindi cha miaka miwili.
Takribani asilimia 70 ya washiriki walikuwa wanawake na wengi wao waliishi na maumivu sugu yanayohusiana au yaliyo hatarini kuhusiana na ugonjwa wa ‘osteoarthritis’ ya goti.
Kwa kutumia vipimo vya juu vya MRI na mbinu za ujifunzaji wa mashine, watafiti walikadiria umri wa ubongo wa kila mshiriki na kuulinganisha na umri wake halisi.
Washiriki waliotoa taarifa za mchanganyiko wenye afya zaidi wa mambo ya kisaikolojia na mtindo wa maisha, walikuwa na ubongo uliokuwa unaonekana kuwa mchanga kwa hadi miaka minane kuliko ilivyotarajiwa.
Kwa upande mwingine, changamoto kadhaa zilihusishwa na ubongo unaoonekana kuwa mzee zaidi, zikiwemo maumivu sugu, kipato cha chini, kiwango cha chini cha elimu na hali ya kudharauliwa kijamii.
Hata hivyo, watafiti walibaini kuwa ingawa athari za changamoto hizo katika kuzeeka kwa ubongo zilipungua kadri muda ulivyopita, manufaa ya tabia chanya za maisha yalikuwa na nguvu zaidi na ya kudumu kwa muda mrefu.
Mienendo mingine iliyohusishwa na kuzeeka kwa ubongo kwa afya bora ni pamoja na kuepuka uvutaji sigara na kudumisha uzito wa mwili wenye afya.
“Ujumbe ni uleule katika tafiti zetu zote,” alisema Kimberly Sibille, profesa mshiriki wa tiba ya mwili na urekebishaji katika Chuo Kikuu cha Florida, aliyeongoza utafiti huo.
“Tabia zinazokuza afya hazihusiani tu na maumivu kidogo na utendaji bora wa mwili. Zinaonekana kwa hakika kuimarisha afya kwa njia ya nyongeza kwa kiwango chenye maana.”
Utafiti huu unaoonyesha kuwa ustawi wa kiakili na chaguzi za mtindo wa maisha, vina mchango muhimu katika afya ya ubongo, hata kwa watu wanaokabiliwa na maumivu sugu au hali mbaya za afya za muda mrefu.
