Dar es Salaam. Kuna baadhi ya mambo ambayo,kwa kawaida, hayapaswi kusemwa na mwanaume kwa mpenzi wake wa kike.
Haya ni maneno au maswali ambayo yanaweza kuathiri uhusiano na kumfanya mpenzi wako ajihisi vibaya, au hata kupoteza mvuto wako kwake.
Kwanza kabisa, sio jambo jema kuomba kibali cha busu kwa mpenzi wako wa kike. Wanawake wengi hupenda kuona busu linatokea kwa asili, wakati unapotaka kufanya hivyo, na si kwa kuuliza kama unaweza.
Unapomuuliza “naweza kukubusu?” unamfanya mpenzi wako aone kama unajiuliza maswali ya kijana mdogo badala ya mwanaume mwenye kujua anachofanya.
Hata kama atakubali, itakuwa ni kwa heshima, lakini sio kwa hamasa. Kama mpenzi wako ni mtu mwenye busara, atajibu “ndiyo”, lakini hiyo itakuwa ni kujibu kwa kistaarabu tu. Kama si hivyo, utapokea jibu la moja kwa moja la “hapana”, na labda atakueleza kwa maneno mengine kuwa ulijionyesha kuwa huna ujasiri wa kufanya jambo hilo mwenyewe.
Mwanaume anapaswa kuwa kiongozi katika uhusiano. Jinsi ya kike imeumbwa kutegemea mwanaume kama kiongozi anayeweza kuanzisha mambo na kuyafanya kirahisi.
Inamshangaza mpenzi wako wa kike pale ambapo kila kitu kinachohitaji uamuzi wako, wewe unahitaji kibali chake ili ufanye jambo fulani. Kwa mfano, kama unataka kumchukua mpenzi wako “out”, hakuna haja ya kumuuliza, “Je, naweza kukutoa out?”
Hili litamfanya akufikirie kuwa bado hujafikia hatua ya kuwa mwanaume mwenye ufanisi. Badala yake, mwanaume anayetegemewa kufanya hivyo ni yule ambaye anapendekeza wapi wangeweza kwenda, na kama kuna maoni tofauti, watakubaliana kwa pamoja.
Kwa mfano, unaweza kusema, “Mpenzi, kuna sehemu nimeiona ambayo ningependa kwenda nayo, unaonaje tukitembelea wikiendi hii?” Hii inatoa picha ya mwanaume mwenye maono na ambaye anajua alichokitaka, huku akimuachia mpenzi wake nafasi ya kutoa mawazo yake.
Ni muhimu pia kujua kwamba, unapokuwa na mpenzi wako wa kike, usizingatie sana mali zako au hali yako ya kifedha. Kusema mara kwa mara kuhusu gari lako, nyumba yako, kazi yako, au mali zako nyingine, kunaweza kumfanya mpenzi wako wa kike aone kwamba unatafuta kuthibitisha kuwa wewe ni mtu muhimu.
Hii inaweza kumfanya akuweke kwenye kundi la wanaume wasio na maadili ya kweli ya kimapenzi, kwani anakiona kuwa unatafuta kuonekana tu badala ya kuonyesha upendo wa dhati.
Ukiona mwanamke anavutiwa na hadithi zako za mali, ujue kuwa yeye ni mmoja wa wale wanaotafuta “faida” kutoka kwako. Mpenzi anayekupenda kwa dhati atavutiwa na wewe kwa kile unachomuonesha kwa ndani, na si kwa kile unachomiliki.
Kwa upande mwingine, wanawake wengi hupenda mwanaume mwenye mpangilio wa maisha. Hii ni muhimu, kwa sababu wanawake wanapenda kuwa na uhakika kuwa mwanaume wao anaweza kupanga mambo na kutekeleza uamuzi kwa ustadi.
Hivyo, usifanye jambo lolote linaloonyesha kuwa hujawaza mambo yako au hauko na mpangilio. Kwa mfano, wakati unapozungumzia kwenda “out”, hakikisha umejiandaa na mpango mzima wa kile mtakachofanya.
Usiruhusu hali ya kuwa tu mmeenda sehemu na kisha kila mtu kukaa kimya au kujitenga na mwingine kwa kutafuta shughuli nje ya mazingira yenu. Hii itamfanya mpenzi wako kujua kuwa huwezi kutoa nyakati za furaha katika uhusiano wenu.
Kuna sentensi nyingine ambayo wanawake wengi hawapendi kusikia, ambayo ni kuuliza “Je, unanipenda?” au “Je, unavutiwa na mimi?” Ingawa pengine mwanamke anaweza kukuuliza swali hili bila kumaanisha kumfanya uonekane dhaifu, kwa mwanaume, swali hili linaweza kutoa picha kwamba hujajiamini.
Mwanaume anayehitaji kuthibitisha upendo wake kwa kuuliza swali kama hili anajiweka katika nafasi ya udhaifu. Hii inamfanya mwanamke ajihisi kama huwezi kuwa na uhakika kuhusu hisia zako kwake. Hivyo, hata kama hujui wazi kama unampenda au la, ni vyema kudumisha hali ya kujiamini na kumwonyesha upendo wako kwa matendo na si kwa maswali.
Pia, usiulize maswali kuhusu mawasiliano kama vile “Nilituma ujumbe wa simu, kwa nini hukupokea?” Swali hili linaweza kumfanya ajihisi kuwa unapenda kumchunguza na kumuhukumu kwa mambo ya kibinafsi.
Wanawake wengi hawapendi kujisikia kuwa wanahukumiwa kwa kufanya vitu vya kawaida kama kutochelewa kujibu ujumbe. Badala yake, jaribu kuendelea na mazungumzo yako kwa njia ya kawaida na usimfanye ajihisi kuwa ni lazima aeleze kila jambo analofanya.
Kwa kumalizia, mambo haya yaliyoainishwa ni baadhi ya vitu ambavyo, kwa kawaida, huathiri uhusiano na kuleta mivutano isiyohitajika.
Ikiwa mwanaume atajitahidi kuepuka kuzungumza kuhusu vitu hivi, na badala yake atazingatia kuonyesha upendo wa dhati, mpangilio, na ujasiri katika uhusiano, atakuwa na uhusiano bora na mpenzi wake wa kike.
