MWANARIADHA maarufu nchini, Alphonce Simbu, ameendelea kuonyesha kiwango cha juu kimataifa baada ya kumaliza nafasi ya pili katika mbio za Kolkata zilizofanyika leo Jumapili huko India.
Katika mbio hizo za kilomita 25, Simbu alitumia saa 1:11:56 kumaliza wa pili nyuma ya Joshua Cheptegei wa Uganda aliyeshinda kwa saa 1:11:49, huku ushindani ukiwa mkali kati ya wanariadha hao bora.
Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Tebello Ramagoana wa Lithunia aliyetumia muda wa 1:11:59, wakati Collins Kipkorir wa Kenya alimaliza nafasi ya nne kwa kutumia muda wa 1:12:02.
Kwa upande wa Wanawake, wanariadha wa Ethiopia walitawala kwa kuchukua nafasi nne za juu, Degitu Azimeraw akiibuka mshindi kwa muda wa 1:19:36 , akifuatiwa na Situme Kabede muda wa 1:20:28, Meselech Alemayehu kwa muda wa 1:20:48 na Kuftu Tayri aliyetumia 1:23:32.
Matokeo hayo yanaendeleza mafanikio ya Simbu mwaka huu, ikiwemo kumaliza nafasi ya pili katika Boston Marathoni Marekani, kushinda medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia yaliyofanyika Septemba Tokyo Japan, na kuweka rekodi ya Mtanzania wa kwanza kushinda marathoni za dunia.
Pia aliingia katika fainali ya mwanariadha bora wa kiume wa mwaka 2025, kipengele cha wanariadha wanaokimbia nje ya uwanja, akiweka rekodi ya kuwa Manzanita wa kwanza kuingia fainali za tuzo zinazoandaliwa na Shirikisho la Riadha la Dunia.
Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), limeeleza mafanikio ya Simbu yanaendelea kuitangaza Tanzania kimataifa na kuchochea maendeleo ya riadha nchini, huku yakitajwa kuwa chachu kwa wanariadha chipukizi kuamini uwezo wao kujituma zaidi.
Rais wa RT, Rogath John amempongeza Simbu kwa kushika nafasi hiyo na kuongeza viongozi wanafurahi kuona mafanikio ya wale wanaowasimamia.
“Simbu ni mpambanaji sana, pongezi kwake na taasisi yake ya Jeshi la Wananchi (JWTZ), pia kocha Anthony Mwingereza ambao wamekuwa naye bega kwa bega kuhakikisha mafanikio mengi zaidi yanapatikana”.
