Lugha tano za mapenzi, yako ipi?

Katika kila uhusiano wa kimapenzi au ndoa, watu wengi hupenda na kupendwa kwa namna tofauti. Wakati mmoja anaweza kuona upendo kupitia maneno matamu, mwingine huhisi upendo anapopewa zawadi au kusaidiwa majukumu ya kila siku. 

Tofauti hizi zinaleta changamoto, hasa pale mpenzi au mwenza anapojaribu kuonyesha upendo, lakini mwenzake hasikii kama anapendwa. 

Dk Gary Chapman, mshauri wa ndoa na mtaalamu wa saikolojia, anaelezea dhana hii kwa undani katika kitabu chake maarufu, The 5 Love Languages (Lugha tano za mapenzi).

Dk Chapman anaeleza kwamba kila mtu ana “lugha kuu ya mapenzi” yaani  njia maalum anayoelewa na kupokea upendo kwa undani zaidi. 

Kuelewa lugha hizi ni njia bora ya kuimarisha uhusiano wowote wa kimapenzi. Makala haya itaeleza kwa kina kila moja ya lugha tano za mapenzi na jinsi zinavyoweza kuboresha maisha ya wapenzi au wanandoa.

Lugha ya uthibitisho wa upendo 

Hii ni lugha ya mapenzi ambayo hutegemea maneno ya kupongeza, kuthibitisha, na kuonyesha shukrani. Watu wenye lugha hii ya mapenzi hupokea upendo zaidi kupitia kauli nzuri kama:

“Umefanya kazi nzuri leo.”

“Asante kwa yote unayofanya.”

Maneno haya huwapa nguvu ya kihisia, huwafariji, na kuwajengea kujiamini. Wapenzi au wanandoa wanaozungumza lugha hii huchanua kwa sifa na hujisikie kutothaminiwa wanapokosolewa au kupuuzwa.

Kuonyesha upendo kwa mtu wa aina hii, unaweza kumtumia ujumbe mfupi wa mapenzi mara kwa mara, ukimweleza  kwa sauti mambo unayoyapenda kuhusu yeye.

Msifu  au mpe shukrani mbele ya watu wengine (ikiwa anapenda hivyo) na epuka kauli za dharau, kejeli au ukosoaji mkali, kwani  hizi huumuumiza sana mtu wa aina hii.

Watu wenye lugha hii ya mapenzi hupokea upendo kupitia uwepo wa kimwili na kihisia wa mwenza wao. Ni zaidi ya kuwa tu karibu kimwili, ni kuwepo kwa makusudi, kwa umakini na kwa kujali.

Wanathamini sana wakati wa mazungumzo ya dhati, kutembea pamoja, kula pamoja bila usumbufu wa simu au runinga, au kushiriki shughuli wanazopenda wote.

Kwao, muda wa pamoja unaonyesha ile dhana ya “Upo hapa kwa ajili yangu, na unanipa kipaumbele.” Kukosa muda pamoja kunaweza kuwafanya wajisikie kusahaulika au kutothaminiwa.

Kuonyesha upendo kwa mtu wa aina hii, pangeni  muda maalum wa kuwa pamoja bila usumbufu, zima simu au weka kando vifaa vya mawasiliano wakati mkiwa pamoja.

Msikilize  kwa makini bila kumkatiza au kumhukumu. Shiriki shughuli ambazo hujumuisha ushirikiano wa kihisia kama kutazama runinga, kupika au kutembea pamoja.

Lugha ya  kupokea zawadi 

Kwa baadhi ya watu, zawadi ni ishara ya upendo. Haijalishi ukubwa au gharama ya zawadi, cha muhimu ni kwamba mtu amefikiria kuwapa kitu maalum. 

Wanaona zawadi kama alama ya fikra na mapenzi. Kila zawadi hubeba maana na kumbukumbu ya kipekee.

Kwa mtu mwenye lugha hii ya mapenzi, kutopokea zawadi kwa nyakati muhimu kama siku ya kuzaliwa, maadhimisho au hata siku ya kawaida kunaweza kuchukuliwa kama kutopendwa au kutothaminiwa.

Ukitaka kutumia lugha hii kwa mwenza wako, toa  zawadi za kawaida mara kwa mara , kama maua, pipi, kutumia ujumbe au kitu chochote anachokipenda.

Aidha, zingatia ubunifu zaidi  katika utoaji zawadi kuliko kuweka mbele thamani ya fedha.

Ubunifu huu unaweza kuwa wa kumpa zawadi kwa kumshtukiza, kumshangaza au hata mbele ya kadamnasi ya watu, lengo likiwa kuongeza msisimko wa zawadi.

Lugha ya kufanya kivitendo

Watu wa aina hii huamini katika msemo: “Vitendo huzungumza zaidi ya maneno.” Kupika chakula, kumsaidia kazi za nyumbani, kumpeleka kliniki, au hata kutengeneza kitu kilichoharibika; haya yote ni njia za kuonyesha upendo kwao.

Wakiwa wamechoka au wanasumbuka, mpenzi au mwenza wao akifanya jambo lolote la kuwasaidia hujiona wanapendwa na kuheshimiwa. Kukosa msaada, ama kuwaachia mzigo peke yao, huwasababishia maumivu na hisia za kupuuzwa.

Jinsi ya kuonyesha upendo kwa mtu wa aina hii: Msaidie bila kusubiri kuombwa; fanya vitu vidogo vinavyoonyesha kujali  kama  kutandika kitanda, kumletea chai, au kumpeleka kazini; kuwa na nia ya kusaidia, si kulazimishwa na  sikiliza mahitaji yake huku ukichukua hatua kabla hajauliza au kuomba.

Kwa watu wa lugha hii, mguso wa kimwili una nafasi ya kipekee sana katika kuwasilisha upendo. Kuguswa, kukumbatiwa, kushikwa mkono, kubusu au hata kukaa karibu tu kunaongeza hisia ya ukaribu. Ni lugha ambayo huleta utulivu wa kihisia na kiroho.

Watu hawa hupokea upendo kupitia mguso, hasa kutoka kwa mtu wanayempenda. Kukosa mguso kunaweza kuwaudhi sana, au kuwafanya wajisikie kutengwa hata kama maneno au zawadi zipo.

Jinsi ya kuonyesha upendo kwa mtu wa aina hii: mkumbatie mara kwa mara, hata bila sababu; mshike mkono mkitembea, au unapomkaribisha nyumbani. Weka mkono kwenye bega lake, au mbusu mnapokuwa pamoja.

Pendelea sana kumgusa mwenza wako kwa namna mbalimbali nje ya mguso wa tendo la ndoa.

Umuhimu wa kuelewa lugha hizi

Kushindwa kuelewa lugha ya mapenzi ya mwenza wako kunaweza kusababisha mawasiliano duni ya kihisia.

Unaweza kuwa unapenda kwa bidii, lakini mwenzako hajisikii kupendwa kwa sababu unatumia lugha tofauti. Mtu wa maneno anapewa zawadi, lakini kwa sababu hajathamini sana zawadi, anahisi kupuuzwa kihisia.

Kwa kuelewa lugha ya mwenza wako, unaweza kuongeza ukaribu na uaminifu katika uhusiano, kuepuka migogoro isiyo ya lazima, kujenga mazingira ya kujaliana na kuheshimiana. Pia kutambua  kwa haraka dalili za maumivu ya kihisia na kujirekebisha kwa upendo.

Unaijuaje lugha ya mwenza wako?

Dk Chapman anapendekeza njia rahisi ya kujua lugha kuu ya mapenzi ya mpenzi au mwenza wako:

Mosi,  jiulize ni kitu gani anacholalamikia mara nyingi?

Pili, chunguza nini anachofanya mara kwa mara kukuonyesha upendo.

Tatu, gundua anachokifurahi  zaidi unapomfanyia.

Baadhi ya watu wanaweza kuwa na mchanganyiko wa lugha mbili au zaidi, lakini mara nyingi kuna moja kuu inayotawala. Kuifahamu na kuitumia ni kama kuwa na funguo ya moyo wa mwenza wako.

Kila mtu anatamani kupendwa kwa njia anayoielewa. Lugha tano hizi, zinatufundisha kuwa upendo haueleweki kwa namna moja tu. 

Ili uhusiano udumu, ni lazima tujifunze lugha ya mapenzi ya wapenzi wetu na kuitumia kwa moyo wote. Hata kama ni maneno matamu, muda wa pamoja, zawadi ndogo, vitendo vya msaada, au mguso wa kimwil, kwani kila lugha ina thamani yake na inaweza kuimarisha sana uhusiano.

Kupenda ni kujitolea. Kupenda ni kujifunza. Na kujua lugha ya mapenzi ya mwenzi wako ni hatua kubwa kuelekea uhusiano wenye afya na furaha ya kudumu.