ALIYEKUWA Kocha wa Fountain Gate, Khalid Adam, amejiunga na kikosi cha African Sports ‘Wanakimanumanu’ cha mjini Tanga, baada ya hivi karibuni timu hiyo kuachana na Sharifu Joseph Ndokezi, kutokana na mwenendo mbaya wa Ligi ya Championship.
Sharifu aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akichukua nafasi ya Kessy Abdallah aliyetimkia kwa maafande wa JKT Queens, amekiongoza kikosi hicho katika mechi tisa, ambapo kati ya hizo alishinda mbili tu, akitoka sare moja na kupoteza sita.
Akizungumza na Mwanaspoti, Adam amesema ni kweli amefikia makubaliano ya kukiongoza kikosi hicho hadi mwisho wa msimu, huku akiomba zaidi ushirikiano kutoka kwa wachezaji na viongozi kwa ujumla, ili kwa pamoja wafikie na kutimiza malengo.
“Kwa nafasi ambayo timu ipo sio nzuri wala mbaya sana kwa sababu gepu la pointi na waliokuwa juu yetu sio kubwa, jambo muhimu ni kuhakikisha tunashirikiana zaidi, kwani hiyo ndio njia bora itakayotusogeza na kututoa tulipo,” amesema Adam.
Kocha huyo wa zamani wa Mwadui, amesema atakaa na viongozi na kuangalia maeneo mbalimbali muhimu ya kuyarekebisha ili mzunguko wa pili uwe ni tofauti na sasa, ingawa anahitaji kuwajenga zaidi wachezaji kisaikolojia kabla ya kufikia huko.
