MSHAMBULIAJI wa Songea United, Raymond Lulendi, amesema licha ya kushirikiana na wachezaji wenzake kuipambania timu hiyo kumaliza nafasi nne za juu, ila malengo yake binafsi ni kuhakikisha pia anakuwa mfungaji bora wa Ligi ya Championship.
Nyota huyo aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea JKU ya visiwani Zanzibar, amefunga mabao sita hadi sasa akiwa na kikosi hicho, akipitwa mawili tu na mshambuliaji kinara wa Gunners ya jijini Dodoma, Abrahaman Mussa aliyefunga manane.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lulendi amesema Ligi ya Zanzibar imempa changamoto ya kujifunza mambo mengi baada ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, japo waliishia raundi ya kwanza, kufuatia kutolewa na Pyramids ya Misri kwa jumla ya mabao 9-1.
“Kwangu ilikuwa kitu kikubwa kucheza Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ingawa hatukuweza kufika mbali kutokana na mpinzani tuliyekutana naye, Ligi ya Zanzibar ni ngumu ila Championship ni zaidi kwa sababu ya ushindani uliopo,” amesema Lulendi.
Mshambuliaji huyo aliyewahi kuichezea pia Fountain Gate kabla ya kutua JKU, amesema licha ya ushindani uliopo hadi sasa, ila atahakikisha anaendelea kujituma zaidi na kutumia vizuri nafasi za kufunga, ili atimize malengo yake aliyojiwekea.
