Mbeya. Mbunge wa Uyole, Dk Tulia Ackson amesema ataendelea kugusa jamii kwa kugharamia bima za afya na sare za shule kwa wanafunzi wenye mazingira magumu, pamoja na kusaidia wazee wasiojiweza.
Akizungumza leo Jumapili Desemba 21, 2025, wakati wa utoaji wa mahitaji kwa wazee katika kata tano za Jimbo la Uyole, Dk Tulia amesema kila kaya imekabidhiwa kilo 20 za mchele pamoja na fedha kwa ajili ya mahitaji ya sikukuu.
Mbunge wa Uyole ,Dk Tulia Ackson akisalimiana na wazee wenye uhitaji katika Kata ya Mwasanga muda mfupi baada ya kugawa mahitaji kwa ajili ya sikukuu.Picha na Hawa Mathias
Amesema hatua hiyo ni mwanzo wa mpango mpana wa kuwafikia walengwa walioainishwa kupitia mbio za bendera za Tulia Trust na kuendelea kuongeza kiwango cha msaada kila mwaka.
Mbunge wa Uyole Dk Tulia Ackson akizungumza na wananchi
“Kazi ndio inaanza. Tutaendelea na bima za afya, sare za shule na mahitaji mengine kwa wenye uhitaji mkubwa,” amesema.
Diwani wa Kata ya Mwasanga, Brandy Nelson, amesema Dk Tulia amekuwa mfano wa uongozi unaogusa wanyonge, huku baadhi ya wananchi wakimtaja kama kiongozi mwenye moyo wa kujitolea.
Baadhi ya wazee ambao wamekabidhiwa mchele kilo ishirini kila mmoja kwa ajili ya kusherekea sikuu za mwisho wa mwaka.Picha na Hawa Mathias
Akizungumzia misaada hiyo, Atupele Mwaisumo amemtaja Dk Tulia ni mwanamke jasiri ambaye ni jicho la wananchi wanyonge.