Mbarali. Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya, imejipanga kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya ndani na kuwachukulia hatua na watumishi watakaobainika kuhujumu miradi ya maendeleo.
Hatua hiyo imekuja kufuatia miaka kadhaa halmashauri hiyo kushindwa kufanya vizuri kwenye makusanyo ya ndani licha ya kutegemea asilimia 80 kutoka kwenye chanzo cha sekta ya kilimo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbarali, Raymond Mweli leo Jumapili Desemba 21,2025, wakati akizungumzia mrejesho wa kikao kazi kilichofanyika Ijumaa iliyopita.
Kikao hicho kilihusisha wakuu wa idara na watendaji wa Serikali sambamba na kuweka mikakati ya kuboresha miradi ya maendeleo .
“Nimewaeleza kila mmoja atekeleze majukumu yake katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani,lakini kama kuna eneo haliendi vizuri kama mkurugenzi siwezi kucheka na mtu anayetaka kuturudisha nyuma kwa kutuvuta shati,”amesema.
Amesema katika hilo tayari wapo watumishi ambao wamechukuliwa hatua kutokana na kukwamisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa makusudi.
“Lakini pia nimetoa katazo na onyo kwa watendaji ni mwiko kuwa na miradi viporo kutokana na Serikali kutoa fedha nyingi za kutekeleza sambamba na kutopokea sababu zisizo za msingi ,”amesema.
Katika hatua nyingine,Mweli ametoa maelekezo kwa wakuu wa idara kuwajibika ipasavyo na kushirikisha watendaji wa kata na vijiji ili kufikia malengo.
Mweli amesema wameweka mikakati ya utaratibu wa kutoa taarifa za kila mwezi katika ofisi ya mbunge kuhusiana na hali ya makusanyo na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa lengo la kuongeza jicho la kulinda na kusimamia masilahi ya umma.
Mweli ameonya watumishi wa Serikali kuachana na lugha mbaya kwa wananchi badala yake kutatua changamoto hususani za ardhi kama sehemu ya kutekeleza maagizo ya Serikali.
Katika hatua nyingine Mweli amesema wanatarajia kuanza ugawaji wa matrekta madogo 76 kwa wakulima ambayo yametolewa kwa lengo la kuboresha tija ya uzalishaji.
Kwa upande wake Mbunge wa Mbarali, Bahati Ndingo amesisitiza kuwajibika kutumikia wananchi katika kutekeleza maagizo ya Serikali.
Ndingo amesema ataanza utaratibu wa kufanya ziara maeneo mbalimbali kuona kama shughuli za Serikali zinatekelezwa ipasavyo, kutatua na kusikiliza kero za wananchi.
Kuhusu uhaba wa watumishi, Ndingo amesema tayari kuanzia Januari 2026,kuna mchakato wa Serikali kuanza kutoa ajira na kusisitiza atasimamia kuhakikisha nao ni wanufaika katika kada mbalimbali .
