MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar, Mlandege, imetozwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la mashabiki wa timu hiyo kufanya vurugu kwa kurusha chupa uwanjani wakati mechi ikiendelea.
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari leo Jumapili Desemba 21, 2025 na Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Zanzibar, Issa Chiwile, imesema katika kikao kilichofanyika Desemba 17, 2025, kamati ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya ligi hiyo ikiwemo mechi namba 100 kati ya Mlandege dhidi ya KVZ.
Mechi hiyo iliyochezwa Desemba 16, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A uliopo Unguja, saa 10:15 jioni, kamati imepitia ripoti za wasimamizi na mwenendo mzima wa mechi hiyo.
Kamati imebaini kuwa katika dakika ya 64, mechi hiyo ilisimama baada ya kutokea vurugu ambapo mwalimu wa viungo wa Mlandege, Abdillah Abdulla alionyeshwa kadi ya njano iliyofanya kutoridhika na uamuzi huo.
Mashabiki wa Mlandege walianza kurusha chupa, kitendo ambacho ni utovu wa nidhamu na kosa kisheria chini ya sura ya 20 ya kanuni ya mashindano ya 2025-2026.
“Hivyo timu ya Mlandege imetozwa faini ya Sh1 millioni kwa kosa la wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kurusha chupa uwanjani wakati wa mchezo huo,” imesema taarifa hiyo.
Pia, mwalimu wa viungo wa timu hiyo, Abdillah Abdulla amepewa onyo kwa utovu wa nidhamu aliouonesha dhidi ya waamuzi, adhabu hiyo imetolewa chini ya sura ya ya 20 ya kanuni ya mashindano ya 2025-2026.
