Tanzania, India zaingia makubaliano kuendeleza tiba asili

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania na India zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) yenye lengo la kuibua, kukuza na kulinda tiba asilia katika mifumo ya kisheria na kidijitali, hatua iliyopongezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kama mchango muhimu katika kuimarisha mifumo ya afya duniani.

Makubaliano hayo yamesainiwa jana, Desemba 20, 2025 nchini India mbele ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus, ambapo Tanzania ilitumia fursa hiyo pia kuwaalika wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali kuwekeza katika sekta ya uzalishaji wa dawa, ikiahidi mazingira rafiki na salama ya uwekezaji.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema hatua hiyo ni mwanzo wa kulinda rasmi tiba asilia kisheria na kuifanya kuwa sehemu muhimu ya mifumo ya afya ya kisasa.

“Tunaamini kuwa tiba asilia, inapolindwa na sheria, ikiimarishwa na sayansi, ikiwezeshwa na teknolojia, na kuendeshwa kwa mtazamo wa kibiashara, inaweza kuwa nguzo muhimu ya kimataifa katika kujenga jamii zenye afya bora,” amesema Mchengerwa.

Amesema ujumbe wa Tanzania nchini India ni kujifunza, kushirikiana na kuongoza katika matumizi salama na yenye tija ya tiba asilia, akibainisha kuwa tiba hizo bado ni mhimili muhimu wa huduma za afya ya msingi nchini Tanzania.

Waziri wa Afya Tanzania, Mohammed Mchengerwa akiweka saini ya makubaliano kulia ni Wazir Mkuu, India Narendra Modi

Kwa mujibu wa Mchengerwa, takribani asilimia 60 ya Watanzania hutumia huduma za waganga wa tiba asilia, ama kabla au sambamba na huduma za hospitali za kisasa, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuhakikisha tiba hizo zinathibitishwa kisayansi.

“Uhalisia huu unaonesha wazi kuwa upatikanaji wa ushahidi wa kisayansi si hiari bali ni jambo la lazima,” amesisitiza.

Akizungumzia usalama, ubora na tafiti za tiba asilia, amesema Tanzania inaunga mkono kikamilifu Mkakati wa Kimataifa wa WHO wa Tiba Asilia wa mwaka 2025–2034, hususan katika eneo la kujenga ushahidi wa usalama, ufanisi na ubora wa tiba hizo.

Ameeleza pia kuwa Serikali inaweka kipaumbele katika tafiti za gharama nafuu zinazofanywa katika jamii kwa kushirikiana na taasisi za utafiti za serikali, maabara na vyuo vikuu, huku akisisitiza umuhimu wa mifumo imara ya udhibiti na uhakiki wa ubora ili kuwalinda wagonjwa.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus (Katikati) Waziri wa Afya wa Tanzania Mohammed Mchengerwa na Waziri wa Mkuu wa India, Narendra Modi.

Kuhusu mfumo wa kisheria, Mchengerwa amesema Tanzania imeweka msingi thabiti kupitia Sheria ya Tiba Asilia na Tiba Mbadala Na. 23 ya mwaka 2002, inayotekelezwa na Baraza la Tiba Asilia na Tiba Mbadala. Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha taasisi zake ikiwemo Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

Lengo kuu, amesema, ni kuifanya tiba asilia iwe ya kitaalamu na inayokidhi viwango vya kimataifa vya ubora na usalama, sambamba na kuziunganisha rasmi katika mfumo wa utoaji wa huduma za afya.

“Tanzania imejidhatiti kuingiza tiba asilia katika huduma za afya ya msingi ili kuunga mkono lengo la bima ya afya kwa wote tangu mwaka 2023,” amesema, akiongeza kuwa huduma hizo tayari zinatolewa katika hospitali rasmi, ambapo bidhaa 27 za tiba asilia zilizothibitishwa zinatumika kutibu magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.

Kwa upande wa uchumi, Mchengerwa amesema tiba asilia ni kichocheo cha ubunifu na ukuaji wa uchumi, huku bidhaa 141 zikiwa tayari zimesajiliwa nchini, zaidi ya asilimia 90 zikitengenezwa na wajasiriamali wadogo wa ndani.

Amesisitiza umuhimu wa kulinda haki miliki, maadili na maarifa ya jamii, akibainisha kuwa Serikali inaendelea kuandaa mifumo ya kisheria na kimaadili ili kulinda maarifa ya asili na kuhakikisha mgawanyo wa faida kwa haki.

Akifunga mkutano huo uliowahusisha mawaziri wa afya kutoka zaidi ya nchi 100, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, amesisitiza umuhimu wa kulinda maarifa ya jadi kwa kutumia teknolojia za kidijitali na Akili Unde (AI), akibainisha kuwa teknolojia haitaondoa nafasi ya waganga wa jadi, bali itaongeza na kulinda hekima yao.