Dk Mwigulu ataka mikoa kuchunguza manunuzi ya umma

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, ameelekeza mikoa yote nchini kuanzisha vitengo maalumu vya kuchunguza taratibu za manunuzi na BQ badala ya kusubiri mbio za Mwenge wa Uhuru, hatua inayolenga kulinda ustawi wa huduma na matumizi sahihi ya fedha za umma.

Dk Mwigulu amesema takribani asilimia 70 ya bajeti ya Serikali hutumika kwenye manunuzi na ujenzi, hivyo ni lazima mifumo ya usimamizi iimarishwe ili kulinda fedha zinazotokana na kodi za Watanzania.

Dk Mwigulu ametoa maelekezo hayo leo Desemba 21, 2025, alipokuwa akikagua miradi ya maendeleo wilayani Nachingwea, mkoani Lindi.

“Naagiza kila mkoa uwe na vifaa na wataalamu wanaoweza kubaini kama taratibu za manunuzi zimefuatwa bila kubomoa majengo. Tuko kwenye maandalizi ya bajeti, hivyo ni muhimu kuwa na wataalamu wa kukagua majengo ya aina hii,” amesema Dk Mwigulu

Ameeleza kuwa Serikali imechoshwa na tabia ya kuuziwa mbuzi kwenye gunia, akisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa wataalamu wa kuchunguza BQ na kulinganisha kilichoandikwa na kazi halisi iliyotekelezwa.

“Jengo linaweza kupakwa rangi na kuonekana zuri, lakini bila BQ huwezi kujua kama thamani ya fedha imezingatiwa. Nataka kila mkoa uwe na kitengo na vifaa vya kuchunguza majengo bila kusubiri mbio za Mwenge wa Uhuru,” amesema.

Amesema katika uchunguzi wake amebaini kuwa kipindi cha mbio za Mwenge wa Uhuru huchaguliwa miradi michache iliyo bora ili mikoa ipate sifa, hali inayoficha mapungufu katika miradi mingine.

“Haiwezekani tujitungie mtihani wetu wenyewe halafu tukose makosa. Vitengo hivi vitafuatilia kila jengo ili kubaini maeneo ambayo serikali imetoa fedha lakini hazikutumika ipasavyo,” amesema

Amesisitiza kuwa anapotembelea miradi anahitaji kupata taarifa za BQ, fedha zilizotumika na kama zinalingana na kazi iliyofanyika, akibainisha kuwa Serikali inataka thamani ya fedha ionekane wazi katika kila mradi.

Pia  ameagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads)cna  Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura)  kufanya tathmini ya miradi yote waliyopewa fedha ili kuhakikisha imetekelezwa kwa kuzingatia BQ, akisema kuwa huo ni msingi wa ugatuaji wa madaraka na uwajibikaji.

Baada ya maagizo hayo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisem), Reuben Kwagilwa, amesema ofisi yake itayasimamia kikamilifu maagizo hayo.

“Umetoa maelekezo kwa upande wa Tarura, Waziri Mkuu, nakuhakikishia tutayasimamia,” amesema Kwagilwa.