Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imempunguzia Edward Kinabo dhamana ya gharama za kesi katika shauri la uchaguzi la kupinga ushindi wa Mbunge wa Kibamba, Angellah Kairuki.
Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, Kinabo aligombea ubunge kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na Kairuki (CCM), ambaye sasa ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, aliibuka kidedea.
Kulingana na kifungu cha 140(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, anayefungua shauri kupinga ushindi wa mbunge anatakiwa kuweka Sh5 milioni kwa kila mjibu maombi kama dhamana.
Kinabo amefungua shauri hilo dhidi ya Kairuki kama mjibu maombi wa kwanza, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kibamba kama mjibu maombi wa pili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mjibu maombi wa tatu katika shauri hilo.
Kulingana na sheria, Kinabo alitakiwa kuweka mahakamani jumla ya Sh15 milioni kama dhamana ya gharama za kesi, lakini kifungu kidogo cha (3) cha sheria hiyo kinatoa nafasi kwa asiye na uwezo kuomba kupunguziwa au kupewa msamaha.
Ni kutokana na kuwepo kwa nafuu hiyo, Kinabo aliwasilisha maombi mahakamani ili apunguziwe kiwango hicho. Kwa mujibu wa kiapo chake, alikuwa na uwezo wa kulipa Sh500,000 kwa kila mjibu maombi na jumla ya Sh1.5 milioni.
Hata hivyo, katika uamuzi wake alioutoa Desemba 18, 2025, na kupatikana katika tovuti ya mahakama leo, Jumapili Desemba 21, 2025, Jaji Awamu Mbagwa, baada ya kupitia mawasilisho ya pande zote mbili, alipunguza na kumtaka aweke jumla ya Sh6 milioni.
Jaji Mbagwa amemtaka Kinabo, ambaye anapinga ushindi wa Kairuki kuwa ni batili kisheria kwa kuwa uchaguzi haukuwa wa haki, kuweka mahakamani kiasi hicho ndani ya siku 14 kuanzia Desemba 18 ili kesi iende hatua ya kusikilizwa.
Katika ombi lake kortini, Kinabo, aliyewakilishwa na wakili Paulo Hyera, alieleza kuwa kwa sasa hana kipato kizuri cha kumwezesha kulipa Sh5 milioni kwa kila mjibu maombi na kwamba kiasi kidogo alichokuwa nacho alikitumia kwenye kampeni.
Mbali na hoja hiyo, alisema fedha kidogo aliyokuwa nayo ameitumia pia kulipa mawakala na kwamba anafanya kazi ya Katibu wa Sekretarieti ya Chaumma kwa kujitolea, na hata fedha ya kumlipa wakili amechangiwa na wafuasi wake.
Hata hivyo, Kairuki, kupitia kiapo chake pamoja na kiapo cha Rose Mpeleta, aliyeapa kwa niaba ya Msimamizi wa Uchaguzi na AG, walipinga ombi hilo wakisema hakuwasilisha uthibitisho wowote bali ni maneno matupu.
Kairuki alienda mbali zaidi na kusema muombaji alikuwa ameshindwa kuwasilisha barua rasmi kutoka kwenye chama chake kuthibitisha kuwa alikuwa akijitolea chamani, wala hakuwasilisha taarifa ya benki kuthibitisha anachokisema.
Mpeleta, katika kiapo chake kwa niaba ya wajibu maombi wa pili na wa tatu, alisema taarifa iliyowasilishwa katika ofisi yake na muombaji wakati wa mchakato wa uteuzi wa kugombea ubunge inazungumza tofauti na alichokieleza.
Katika taarifa hiyo, Mpeleta alisema muombaji alieleza kuwa ameajiriwa na Chaumma kama Katibu wa Sekretarieti na Mkurugenzi, na analipwa vizuri.
Mpeleta alieleza pia kuwa muombaji ni mfanyabiashara na Mkurugenzi Mwenza wa kampuni ya Ardhicare na katika kuthibitisha hilo aliambatanisha fomu yake ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea, aliyoiwasilisha kwa msimamizi wa uchaguzi.
Katika usikilizwaji wa maombi hayo uliofanyika Desemba 18, 2025, mjibu maombi wa kwanza aliwakilishwa kortini na wakili Kamara Mpaya, wakati mjibu maombi wa pili na wa tatu waliwakilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ayoub Sanga.
Akijenga hoja za kwa nini mteja wake apunguziwe ada hiyo, wakili Hyera alisema kuwa kulingana na Ibara ya 13(1) na (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, muombaji ana haki ya kufikia mahakama pasipo vikwazo vyovyote.
Aliongeza kusema kuwa kifungu cha 143(3) cha Sheria ya Uchaguzi, kanuni ya 11(1), kinaipa mahakama mamlaka ya kupunguza kiwango cha juu cha ada ya dhamana ya gharama za kesi na kuweka kiwango itakachoona ni busara kuwekwa.
Wakili huyo alisema sheria haijaweka masharti maalumu ya kupunguza au kuondoa kabisa ada hiyo kwa makusudi kabisa, ili mahakama itumie utashi wake, na ni wajibu wa mahakama kupima ni kiasi gani muombaji akiweke kama dhamana.
Akijibu hoja hizo, wakili Mpaya, anayemwakilisha Kairuki, alisema maelezo ya muombaji kuwa hana uwezo wa kulipa Sh5 milioni kwa kila mjibu maombi ni maneno matupu yasiyo na uthibitisho wowote.
Alisema ingawa ni utashi wa mahakama kuamua kiwango kinachopaswa kuwekwa kortini kama dhamana ya gharama za kesi, utashi huo lazima utumike kwa busara, kwa kuegemea ushahidi na vielelezo vinavyothibitisha kutokuwa na uwezo wa kifedha.
Kwa upande wake, wakili Sanga aliunga mkono wasilisho la wakili Mpaya na kuongeza kuwa katika maombi kama hayo, mahakama inatakiwa ipime kama muombaji atoe sababu zitakazoiwezesha mahakama kupima.
Alipinga hoja ya muombaji kuwa takwa la kuweka dhamana hiyo linazuia haki ya kikatiba ya kusikilizwa na mahakama, akisema hoja hiyo haina mashiko kwa kuwa si haki ya moja kwa moja bali lazima ikidhi vigezo vya kisheria.
Wakili Sanga alisema mzigo wa kuthibitisha kutokuwa na uwezo ni wa muombaji na kwamba muombaji hakujibu kiapo kinzani cha mjibu maombi wa pili na wa tatu, hali inayotoa tafsiri kuwa alikubaliana na hoja zilizowasilishwa akipinga uwezo wake.
Katika uamuzi wake, Jaji Mbagwa alisema amepitia kwa umakini mawasilisho ya pande zote mbili na kwamba hoja ya msingi ya kuamua ni kama muombaji ametoa sababu za kuishawishi mahakama kumpunguzia kiwango hicho cha fedha.
Alisema kama sheria inavyotaka, kila anayefungua shauri la aina hiyo anatakiwa kuweka mahakamani Sh5 milioni kwa kila mjibu maombi kama dhamana ya gharama za kesi, hivyo kupunguza au kusamehe ni busara ya mahakama.
“Nakubaliana kabisa na wakili Kamara Mpaya kwamba muombaji ndiye anayewajibika kuipatia mahakama nyenzo za kutosha kwa ajili ya kutekeleza mamlaka na wajibu wake,” alisema Jaji, na kuongeza kusema kuwa:
“Kwa upande mwingine, muombaji ameeleza kuwa yeye anafanya kazi kwa kujitolea hivyo hapati pesa, lakini Mpeleta anasema katika fomu aliyoiwasilisha alieleza ameajiriwa kama Katibu wa Sekretarieti ya Chaumma na Mkurugenzi.”
“Kuhusiana na hilo, naenda sambamba na wakili Mpaya kwamba muombaji alitarajiwa kuwasilisha hati rasmi kuthibitisha kuwa anafanya kazi bila malipo,” amesema.
Jaji alisema ingawa anaona muombaji hajairidhisha mahakama kiasi cha kumruhusu kuweka Sh500,000, lakini kupinga matokeo ya uchaguzi ni haki ya kikatiba ya waleta maombi na ni kielelezo cha demokrasia na utawala wa sheria.
“Yote yaliyozingatiwa hapo juu, na kuweka usawa kati ya haki ya kikatiba ya muombaji ya kupinga matokeo ya uchaguzi, ninaona kwamba amana ya Sh2 milioni kwa kila mjibu maombi itakuwa ya haki,” alisema Jaji Mbagwa.
“Nasema hivyo kwa sababu, kwa maoni yangu, amana ya jumla ya Sh6 milioni itatosha kuonesha dhamira ya kweli ya muombaji ya kupinga matokeo ya uchaguzi, kwa upande mmoja, na inaweza kupunguza gharama za wajibu maombi endapo ombi la uchaguzi litatupiliwa mbali kwa gharama, kwa upande mwingine.”
“Hivyo, muombaji anaamriwa kuweka mahakamani kiasi cha Sh6 milioni ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya uamuzi huu,” alisisitiza Jaji Mbagwa.
