WAZIRI KOMBO ASHIRIKI MKUTANO WA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA AFRIKA NA URUSI NCHINI MISRI

……………

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ameongoza Ujumbe wa Tanzania kushiriki katika Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Urusi uliofanyika tarehe 19 na 20 Disemba, 2025, jijini Cairo, Misri. Mkutano huo ulihudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika, Jumuiya za Kikanda za Afrika pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi. 

Mkutano huo uliofanyika chini ya Wenyeviti Wawili, Mheshimiwa Dkt. Badr Abdelatty, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri na Mhe. Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Shirikisho la Urusi, umetoa nafasi ya nchi za Afrika na Urusi kujadiliana na kukubaliana masuala muhimu yanayogusa maslahi ya pamoja katika nchi zao na katika Umoja wa Mataifa, na Mashirika yake.

 Mawaziri wa Afrika na Urusi wamesisitiza umuhimu wa Umoja wa Mataifa na Mashirika yaliyo chini yake, ikiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufanyiwa marekebisho ili kuongeza uwakilishi wa Afrika, kuimarisha uwajibikaji na ufanisi, kuwa na mfumo wa biashara duniani unaozingatia usawa, na kutoa nafasi sawa kwa kila nchi kushiriki kwa uhuru katika majadiliano na maamuzi muhimu yanayoigusa dunia. 

Katika Mkutano huo Waziri Kombo alipata wasaa wa kutoa Hotuba fupi iliyoakisi uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo, na maeneo ya kimkakati ya ushirikiano yanayoendelea kutekelezwa kati ya Tanzania na Urusi. 

Katika Hotuba yake hiyo pia alisisitiza kuwa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Urusi na mataifa ya Afrika, ulioanza kabla na wakati wa mapambano dhidi ya ukoloni, hauna budi kuendelea, lakini uweke kipaumbele zaidi katika kuongeza ushirikiano wa kiuchumi, hususan katika sekta za kimkakati za miundombinu na usafirishaji, nishati na nishati mbadala, teknolojia, TEHAMA, na afya. Alisitiza kuwa ushirikiano ulioimarishwa katika sekta hizi utasaidia juhudi za Afrika za kupanua Uchumi wake.

Ili kuimarisha usalama wa chakula barani Afrika, Waziri Kombo alisisitiza kuwa kunahitaji uwekezaji zaidi kutoka Urusi katika kilimo, ikiwa ni pamoja na kilimo endelevu, viwanda vya usindikaji wa kilimo, na uzalishaji wa mbolea. 

Jukwaa la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Urusi na Afrika liliundwa mwaka 2023 ikiwa ni sehemu ya maazimio ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Urusi na Afrika uliofanyika mwaka 2023 nchini Urusi, ambao uliazimia kuundwa kwa Jukwaa la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Urusi na Afrika ili Jukwaa hilo lijadili utekelezaji wa Maazimio ya Mikutano hiyo ya Ngazi za Juu. 

Majadiliano ya Urusi na Afrika kwa pamoja yanafanyika ili kuainisha, kujadili na kukubaliana namna ya nchi za Urusi na Afrika zinaweza kuongeza ushirikiano katika maeneo ya kimkakati kama vile uchumi, amani na usalamaa, mapambano dhidi ya ugaidi na uhalifu wa kuvuka mipaka, mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula, na maendeleo endelevu.