Ahoua ajichomoa kikosini Simba, sababu yatajwa

KIKOSI cha Simba kikijiandaa kumpokea kocha mkuu mpya, Steve Barker aliyetambulishwa wikiendi iliyopita kuja kuchukua nafasi ya Dimitar Pantev aliyesitishiwa mkataba baada ya siku 61 tu tangu ajiunge na timu hiyo, kiungo mshambuliaji mmoja nyota wa timu hiyo ameamua kujichomoa mapema.

Simba ilimtangaza Barker aliyekuwa akiinoa Stellenbosch ya Afrika Kusini anayetarajiwa kuingia nchini muda wowote kuanzia leo, lakini mapema Jean Charles Ahoua ameonyesha dalili za kutaka kuachana na klabu hiyo baada ya kugoma kuongeza mkataba mpya wa kuitumikia timu hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zimeliambia Mwanaspoti, kiungo huyo raia wa Ivory Coast katika mazungumzo ya awali ya kutaka kuongezewa mkataba amewaambia wazi mabosi wa klabu hiyo kwamba hana mpango wa kuendelea kuwapo kutokana na kutofurahia kutopewa nafasi ya kucheza.

Mkataba wa Ahoua na Simba unatarajiwa kufikia tamati mwishoni mwa msimu na mabosi wa klabu hiyo walitaka kumuongezea mapema ili kuepuka kumkosa kupitia dirisha dogo kutokana na kuwapo kwa taarifa za kutakiwa na klabu kadhaa ikiwamo Raja Casablanca ya Morocco.

Raja kwa sasa inafundishwa na kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids aliyemsajili nyota huyo msimu uliopita kutoka klabu ya Stella Club d’Adjame ya Ivory Coast na kumaliza kinara wa mabao wa timu hiyo na Ligi Kuu Bara kwa ujumla akiwa na mabao 16 na kuiwezesha Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikipoteza kwa mabao 3-1 mbele ya RS Berkane ya Morocco.

Taarifa zinasema, Ahoua amewaambia mabosi wa Msimbazi kwamba, hayupo tayari kusaini mkataba mpya na Simba kwa wakati huu, akieleza kuwa anahitaji changamoto mpya nje ya Tanzania baada ya msimu huu kuanza bila ya kuwa katika kikosi cha kwanza kwanza na kutumika kwa dakika chache akifunga bao moja tu kupitia mechi tano ilizocheza timu hiyo katika Ligi Kuu Bara.

Vyanzo vya ndani vinaeleza kuwa, mabadiliko ya mifumo ya uchezeshaji, pamoja na presha ya ushindani ndani ya kikosi, yamechangia kushuka kwa makali ya Ahoua ukilinganisha na msimu uliopita.

Pamoja na hali hiyo, taarifa zinaeleza Ahoua bado anaamini uwezo wake haujapungua, bali mazingira ya sasa hayampi uhuru ule aliokuwa nao awali chini ya kocha Fadlu anayeripotiwa kuvutiwa na nyota huyo na kulipelekea jina kwa mabosi wa Raja AC, ili imsajili na kuungana naye kwa mara nyingine.

Inaelezwa, Fadlu anamwona Ahoua kama mchezaji sahihi wa kuimarisha kikosi cha Raja, akiamini anaweza kuonyesha makali kama aliyoyaonyesha msimu uliopita akiwa chini yake, lakini ikidaiwa pia Ahoua ana ofa kadhaa mezani, zikiwamo za klabu za nyumbani kwao Ivory Coast na Uarabuni.

Kwa upande wa Simba, hali hii imeanza kuupa uongozi presha ya kufanya uamuzi wa haraka kumuuza pindi dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa Januari Mosi 2026 ili kuepuka kumpoteza bure mchezaji huyo kwani yeye ni miongoni mwa wachezaji ambao mikataba yao ipo ukingoni kwa sasa.