KOCHA wa maafande wa Tanzania Prisons, Mkenya Zedekiah ‘Zico’ Otieno, ameanza mipango ya kuisuka upya timu hiyo katika dirisha dogo litakalofunguliwa Januari Mosi, 2026, huku akimfuatilia aliyekuwa mshambuliaji wa Pamba Jiji, George Mpole.
Chanzo kutoka katika timu hiyo, kimeliambia Mwanaspoti, Zedekiah anahitaji mshambuliaji mpya wa kuongeza nguvu, baada ya kuondoka kwa Abdulkarim Segeja, ili akasaidiane na nyota wengine pia kikosini wakiwamo, Jeremiah Juma na Oscar Mwajanga.
Mtoa taarifa huyo, aliliambia Mwanaspoti uongozi wa timu hiyo unafanya mazungumzo ya kumpata Mpole katika dirisha hili dogo la Januari, baada ya mshambuliaji huyo kutokuwa na klabu yoyote tangu alipoachana na Pamba Jiji, Januari 7, 2025.
“Mazungumzo hayo yapo ila moja ya vitu ambavyo tunafanyia kazi kwa kushirikiana na benchi la ufundi ni kujiridhisha tu kwanza juu ya fitinesi yake kwa sababu amekua nje kwa muda bila ya kucheza mechi za kiushindani,” kilisema chanzo hicho.
Msimu wa 2024-2025, Mpole akiwa na Pamba, aliifungia mabao mawili ya Ligi Kuu Bara, japo msimu wa 2021-2022, ndio uliokuwa mzuri zaidi akiichezea Geita Gold, alipokuwa mfungaji bora wa Ligi, baada ya kufunga mabao 17.
Nyota huyo aliyewahi kuzichezea pia, Real Nakonde ya Zambia, FC Saint Eloi Lupopo ya DR Congo na Mbeya City, ni miongoni mwa washambuliaji wanaohitajika na kikosi hicho cha maafande wa Prisons, ili kuongeza nguvu katika eneo hilo msimu huu.
Katika mechi saba ilizocheza Prisons msimu huu katika Ligi Kuu Bara ambapo inashika nafasi ya 14 kwa pointi saba, safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho imefunga mabao matatu tu, jambo linaloufanya uongozi kusaka mshambuliaji wa kuongeza nguvu.
