WAKATI ikielezwa uongozi wa Singida Black Stars unaweza ukaachana na winga nyota wa timu hiyo, Ayoub Lyanga anayewindwa na Mbeya City, mabosi wa kikosi hicho wameanza mazungumzo na kiungo mshambuliaji wa TRA United, Ramadhan Salum Chobwedo.
Chobwedo aliyejiunga na TRA (zamani Tabora United) katika dirisha dogo la Januari 2024, akitokea KenGold ya Mbeya iliyopo Ligi ya Championship msimu huu, anaonekana mbadala sahihi wa Lyanga kutokana na kiwango chake bora.
Nyota huyo ameonyesha kiwango kizuri na timu hiyo tangu ajiunge nayo akiwa ni mchezaji wa kikosi cha kwanza, ambapo kwa sasa mabosi wa Singida wanaifukuzia saini yake, ingawa hadi sasa hakuna makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande mbili.
Kiongozi mmoja wa TRA United, aliliambia Mwanaspoti ni kweli mchezaji huyo anahitajika na Singida, ingawa sio rasmi kwa sasa kwa sababu hakuna makubaliano yoyote kati ya klabu hizo mbili yaliyofikiwa, hivyo, ni tetesi tu.
“Mchezaji pekee aliyeondoka baada ya mkataba wake kuisha na alituaga vizuri tu ni mshambuliaji, Emmanuel Mwanengo, ila wengine hakuna makubaliano tuliyofia, lengo letu ni kubakia na wachezaji wetu wote muhimu pia,” kilisema chanzo hicho.
Nyota huyo aliyewahi kuichezea TMA ya jijini Arusha inayoshiriki Championship msimu huu kabla ya kucheza Ligi Kuu Bara, hadi sasa amefunga bao moja la Ligi, katika ushindi wa TRA United wa 1-0, dhidi ya Tanzania Prisons, Novemba 22, 2025.
