BEKI wa kushoto wa Bigman, Adeyum Saleh, amesema siri ya timu hiyo kufanya vizuri ni kwa sababu ya wachezaji kuelewana aina ya uchezaji, hali ambayo ilikuwa ngumu kwao mwanzoni mwa msimu huu kutokana na wengi wao walikuwa bado hawajuani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Adeyum aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu baada ya kuachana na Geita Gold, amesema mechi za mwanzo walipata shida kuelewana kwa sababu kulikuwa hakuna pia muunganiko kati yao, ingawa kwa sasa mambo ni mazuri.
“Wachezaji wengi ni wapya hapa na tulikutana tukiwa hatujafanya maandalizi ya msimu (Pre Season) kwa muda mrefu pamoja, hali hiyo ilisababisha kupoteza mechi nyingi za mwanzoni, japo tunashukuru kwa sasa tumezoeana vizuri,” amesema Adeyum.
Nyota huyo aliyewahi kuwika na timu mbalimbali zikiwemo za, Yanga, Coastal Union, Stand United, Kagera Sugar na Dodoma Jiji, amesema licha ya ushindani uliopo ila wataendelea kupambana kwa sababu gepu la pointi sio kubwa na washindani wao.
Bigman imecheza mechi 10, kabla ya ile ya jana nyumbani dhidi ya Mbeya Kwanza, ambapo timu hiyo imeshinda minne, sare miwili na kupoteza minne, ikifunga mabao manane na kuruhusu saba, huku kikosi hicho kikiwa nafasi ya tisa na pointi 14.
