ULEGA ATOA MAELEKEZO MAPYA BARABARA YA AMANI MAKORO

…………

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewataka wakandarasi kuweka kipaumbele cha utu na kuondoa kero kwa wananchi kila wanapopewa kazi za ujenzi hapa nchini kwani huo ndio mwelekeo wa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan. 

Akizungumza mkoani Ruvuma, Ulega amesema kila kwenye kazi ya ujenzi, ni muhimu kwa mkandarasi kufanya kwanza mambo yatakayorahisisha maisha ya watu na kulinda utu wao badala ya kufikiria tu kumaliza ujenzi wa barabara. 

“Kama umepewa kazi ya ujenzi, fikiria unawezaje kurahisisha maisha ya watu? Kama unaweza kuweka kalvati kuzuia maji yasiingie kwenye nyumba za watu, weka kwanza kalvati halafu endelea na ujenzi.,” amesema Ulega. 

Ulega ameyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kitahi – Amani Makoro – Ruanda hadi Bandari ya Ndumbi (km 85) kwa kiwango cha lami unaotekelezwa na kampuni ya China Railway Seventh Group (CRSG).

Waziri Ulega amefanya ziara hiyo baada ya maelekezo ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye alionesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo ingawa serikali tayari imemlipa mkandarasi huyo.

Akiwa katika eneo la mradi, Ulega alimtaka mkandarasi huyo kujenga kwa kasi bila kuchelewa na kwamba serikali haipendi kuona wananchi wakiteseka kwa mambo ambayo yanaweza kumalizwa. 

Waziri Ulega amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anajenga vivuko vya wananchi, kuongeza upana wa mitaro na urefu wa makalavati katika eneo la Amani Makoro sambamba na ufungaji wa taa za barabarani kuanzia Kitahi hadi Amani Makoro ili kurahisisha shughuli za biashara kufanyika usiku na mchana.

“Yapo maelekezo mahususi ya Mheshimiwa Rais Dkt.  Samia Suluhu Hassan atakapomaliza kazi anataka kuona wananchi wake wajawe na nyuso za furaha na tabasamu hivyo basi hakikisheni ujenzi wa barabara na madaraja unazingatia utu wa wananchi ili tutatue changamoto na kuleta tabasamu”, amesema Waziri Ulega

Waziri Ulega pia amemuelekeza Meneja wa TANROADS  Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha anatengeneza maegesho ya malori katika hifadhi ya barabara eneo la Amani Makoro ili magari hayo yasisimame pembezoni mwa barabara na kuharibu miundombinu hiyo.

Naye, Meneja wa TANROADS mkoa wa Ruvuma Mhandisi Salehe Mkwama ameeleza kuwa mradi wa barabara hiyo unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 60.4 na umegawanyika katika sehemu tatu.

Sehemu ya kwanza ya kilometa 5 kuanzia Kitahi hadi Amani Makoro imekamilika na sasa Mkandarasi anaendelea na Sehemu ya pili kuanzia Amani Makoro hadi Ruanda (km 35) ambayo imefikia asilimia 41 ya utekelezaji wake.

Ameeleza kuwa sehemu hiyo ya pili ilipaswa kukamilika mwezi Disemba 2025 lakini imeshindakana kutokana na changamoto mbalimbali ambazo baadhi tayari Serikali imeshazichukuliza hatua na zingine zinaendelea kuchukuliwa za mara kwa mara ili kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo mwezi Aprili, 2026.

Mhandisi Salehe amemuahidi Waziri Ulega kuyafanyia kazi maelekezo yote aliyoyatoa ikiwemo ya ufungaji wa taa za barabarani na kumueleza kuwa mradi huo una jumla ya taa 880 ambazo zitafungwa katika maeneo yote yenye miji ya wananchi na katika madaraja makubwa kwa ajili ya ulinzi na usalama wa wananchi .

Akitoa maelezo yake, Afisa Mwajiri kutoka kampuni ya CRSG Themistocles Rugabela, alimwomba Ulega  kumfikishia salamu za kumuomba radhi Waziri Mkuu na kuhusu kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kufanya kazi usiku na mchana kukamilisha ujenzi huo kwa kasi na ubora unaotakiwa.

Hapo awali, wananchi wa eneo la Amani Makoro walimuomba Waziri Ulega kutatua kero ya vivuko vya kupita wananchi katika barabara hiyo ili watoto wa shule na wananchi wengine waweze kuvuka kwa urahisi.

Mwisho

 

<