ZFDA yakamata kilo 1,232 za nyama iliyoisha muda wake

Unguja. Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imekamata kilo 1,232 za nyama zilizoisha muda wake kwenye moja ya vyumba vya kuhifadhia bidhaa hiyo katika Kampuni ya JM Investment iliyopo Fuoni Ijitimai, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Miongoni mwa kilo hizo, vipo vipapatio vya kuku boksi 55, kuku paketi 254, vidali vya kuku paketi 58 na nyama ya ng’ombe paketi 12.

Akizungumzia hilo leo, Desemba 22, 2025, Mkaguzi wa Chakula kutoka ZFDA, Dk Thamra Khamis Talib, amesema wakati maofisa hao wakifanya ukaguzi wa kawaida waligundua bidhaa hiyo ikiwa imehifadhiwa huku ikiwa katika vifungashio visivyo vya asili.

Amesema kubadilishwa kwa vifungashio kunahusisha kampuni hiyo kubadilisha tarehe ya mwisho ya matumizi, jambo ambalo si sahihi.

Amesema bidhaa hiyo itabaki chini ya ZFDA kwani si salama kwa matumizi ya binadamu, na mmiliki wa bidhaa hiyo atachukuliwa hatua za kisheria kwa kushindwa kumlinda mtumiaji.

“Vipapatio vinavyotoka Dubai kilo 420 vimebadilishwa vifungashio na taarifa zake, na baadhi ya bidhaa nyingine zimebadilika rangi ya asili. Hii inaashiria kuwa bidhaa hizi hazifai kwa matumizi ya binadamu, ni lazima tukaziteketeze, na tumemtaka mfanyabiashara kuja ofisini kwa taratibu za uteketezaji kwa gharama zake. Adhabu nyingine pia zitafuata,” amesema Dk Thamra.

Vilevile, amewataka wafanyabiashara kuwa wazalendo na kuendelea kushirikiana na ZFDA ili kumlinda mtumiaji, huku akibainisha kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa atakaekiuka kinyume.

Amesema ZFDA itaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhakikisha wanakuwa na uelewa wa kutosha juu ya masuala haya na kushiriki kikamilifu katika kufichua wafanyabiashara wa aina hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya JM Investment, mmoja wa watendaji wa kampuni hiyo (hakutaka kutaja jina) amesema wameendelea kuhifadhi bidhaa hiyo si kwa matumizi ya binadamu, bali walitumia kidogo-kidogo kulisha mbwa waliopo katika kampuni hiyo. Pia, hawakujua kwamba kufanya hivyo ni kosa kisheria.

“Sisi tulikua hatuuzi nyama hii, ilikua tunawalisha mbwa. Kosa letu ni kuwa hatukuwajulisha ZFDA kuwa tumehifadhi bidhaa kwa ajili ya chakula cha wanyama, na tunaahidi hawatorejea tena,” amesema.