Kongani ya viwanda Kahama kuwa kitovu cha uzalishaji, usambazaji ukanda wa SADC

Shinyanga. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema kongani maalumu ya viwanda inayojengwa katika eneo lililokuwa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi, wilayani Kahama mkoani Shinyanga, inatarajiwa kuwa kitovu kikubwa cha uzalishaji na utoaji wa bidhaa na huduma kwa migodi iliyopo kusini mwa Jangwa la Sahara ndani ya ukanda wa SADC.

Amesema katika kongani hiyo, zaidi ya viwanda 15 vinavyohusiana na uzalishaji wa bidhaa za migodini vinatarajiwa kujengwa, huku wawekezaji zaidi ya 30 wakionesha nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali. Uwekezaji huo unalenga kuchochea uchumi wa mtu mmoja mmoja, Mkoa wa Shinyanga na Taifa kwa ujumla.

Aidha, amesema katika awamu ya kwanza, viwanda vitatu vya kuzalisha vilipuzi vitajengwa ili kuhudumia migodi mikubwa pamoja na wachimbaji wadogo, kutokana na umuhimu mkubwa wa bidhaa hiyo katika shughuli za uchimbaji wa madini.

Waziri wa madini, Anthony Mavunde akizungumza na wanahabari leo Desemba 22, 2025 baada ya kukagua kongani maalumu ya viwanda ulipokuwa mgodi wa uchimbaji wa madini ya dhahabu wa Buzwagi. Picha na Amina Mbwambo

Waziri Mavunde amesema hayo leo Jumatatu, Desemba 22, 2025, alipotembelea na kukagua maendeleo ya eneo la kongani ya viwanda ya Buzwagi wilayani Kahama, akieleza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha fedha zinazotumika kununua bidhaa na huduma za migodini kutoka nje ya nchi zinabaki ndani ya nchi na kuwanufaisha Watanzania, sambamba na kuvutia wawekezaji zaidi wa ndani na nje.

Amesema zaidi ya Sh5.1 trilioni hutumika kila mwaka kuagiza bidhaa na huduma za migodini kutoka nje ya nchi, kiasi ambacho ni kikubwa kuliko mapato ya kodi yanayokusanywa kutoka kwenye migodi hiyo.

Amesisitiza kuwa Serikali inalenga kuifanya Kahama kuwa kitovu cha utoaji wa huduma na bidhaa za migodini si kwa Tanzania pekee, bali kwa ukanda mzima wa kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mavunde amesema hatua hiyo itabadilisha uchumi wa Kahama na Taifa kwa ujumla.

Akizungumzia athari za kufungwa kwa mgodi wa Buzwagi, Waziri Mavunde amesema ulikuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo na mapato ya Wilaya ya Kahama kwa zaidi ya miaka 16.

Hata hivyo, amesema kubadilishwa kwa matumizi ya eneo hilo na kuwa kongani ya viwanda kutatoa fursa mpya za ajira na shughuli za kiuchumi kwa wananchi.

Waziri wa madini, Anthony Mavunde akiongozana na kamati ya usalama ya mkoa wa Shinyanga leo Desemba 22, 2025 kukagua kongani maalumu ya viwanda – Buzwagi. Picha na Amina Mbwambo

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), Gilead Teri, amesema uwekezaji katika kongani ya Buzwagi umeanza kuvutia kampuni kubwa za ndani na nje ya nchi, huku baadhi yao tayari wakisaini mikataba ya kuanzisha shughuli za uzalishaji.

Amesema utoaji wa leseni unasimamiwa kwa haraka na ufanisi, na mwekezaji yeyote atakayewasilisha maombi atapatiwa leseni ndani ya saa 24.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema eneo la Buzwagi lenye ukubwa wa hekta 1,333 tayari lina miundombinu muhimu, ikiwemo umeme na vyanzo vya maji, hali inayolifanya kuwa fursa adhimu kwa Watanzania kuwekeza.

Mkuu huyo wa mkoa amesisitiza kuwa Shinyanga imejipanga kuweka mazingira wezeshi na kutoa kipaumbele kwa wawekezaji wa ndani, ili kuhakikisha kongani hiyo inafanikiwa na kuwa mfano wa kuigwa nchini.