Maswa. Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Maswa (Mauwasa) imeanza kuchukua hatua za kurejesha maeneo yote yaliyovamiwa na shughuli za kibinadamu katika baadhi ya vyanzo vyake vya maji, ikiwemo mito iliyochepushwa.
Vyanzo hivyo hupeleka maji katika bwawa la New Sola, ambacho ni chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa mji wa Maswa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Mhandisi Nandi Mathias, akizungumza leo Jumatatu Desemba 22, 2025, mjini Maswa mkoani Simiyu, amesema mamlaka hiyo imebaini uwepo wa mito iliyotengenezewa matuta, hali inayosababisha maji kushindwa kupita kwenye mkondo wake wa asili na badala yake kujaa kwenye madimbwi.
Pia amesema baadhi ya watu wanafanya shughuli za kibinadamu, kama kilimo, na kusababisha udongo kuporomokea kwenye bwawa hilo, jambo linalopunguza kina cha maji.
“Tumebaini baadhi ya mito imezibwa kwa kutengenezewa matuta. Maji hayapiti kufuata mto kama ilivyokusudiwa, bali yanajaza madimbwi na matuta hayo, jambo linalopunguza kwa kiasi kikubwa maji yanayoingia katika bwawa la New Sola,” amesema Mathias.
Amesema mamlaka hiyo imeamua kutumia nguvu kazi na mitambo kusawazisha na kuondoa matuta hayo ili kuruhusu maji kupita kwa uhuru na kurejesha mtiririko wa asili wa mito inayoelekea bwawani.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, maeneo yaliyoathiriwa ni pamoja na Mwanguhi hadi Zanzui, ambako kwa muda mrefu kumeshuhudiwa shughuli za kibinadamu, zikiwemo kilimo na ujenzi, zikifanyika kinyume na sheria za uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Hata hivyo, Mauwasa imetoa wito kwa Ofisi ya Bonde la Ziwa Victoria kufuatilia kwa karibu na kuchukua hatua za kudumu katika kulinda chanzo cha maji cha Bwawa la New Sola. Imeelezwa kuwa ofisi hiyo ndiyo yenye dhamana kisheria ya kusimamia na kulinda rasilimali za maji kwa masilahi ya wananchi wa mji wa Maswa.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Mkazi wa Mwanguhi, Juma Maduhu, amesema ulinzi wa chanzo hicho hauwezi kufanywa na mamlaka hiyo pekee, hivyo kuna umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na taasisi husika.
“Ulinzi wa chanzo hiki hauwezi kufanywa na Mauwasa pekee. Tunaiomba Ofisi ya Bonde la Ziwa Victoria kusimamia kikamilifu eneo hili ili kulinda haki ya wananchi kupata maji safi na salama,” amesema Maduhu.
Mkazi mwingine wa Zanzui, Rehema Nyambura, ameeleza wasiwasi juu ya uharibifu wa vyanzo vya maji ambao umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu bila kuchukuliwa hatua madhubuti.
Nyambura amesema shughuli za kibinadamu, kama kuziba mito kwa ajili ya kilimo, zimekuwa zikifanyika bila udhibiti, hali iliyoathiri upatikanaji wa maji.
“Tulikuwa tunaona watu wanaziba mito kwa ajili ya mashamba, tukadhani hakuna madhara. Sasa maji yamepungua hata kwenye visima. Hatua hii imechelewa, lakini ni muhimu,” amesema.
Amesisitiza ulinzi wa vyanzo vya maji unapaswa kupewa kipaumbele na taasisi zote zinazohusika. Amesema usimamizi wa karibu kutoka Ofisi ya Bonde la Ziwa Victoria utasaidia kuzuia uharibifu wa mito na vyanzo vya maji, kwani wananchi watajua kuwa kuna udhibiti wa kutosha.
Kwa upande wake, Mauwasa imewataka wananchi kuacha mara moja kufanya shughuli zozote za kibinadamu katika maeneo ya vyanzo vya maji, ikisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka maagizo hayo.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa hatua hizo zinalenga kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji safi na salama kwa wakazi wa mji wa Maswa.
