MSHAMBULIAJI wa zamani wa Pamba Jiji, George Mpole ametaja sababu ya washambuliaji wa ndani kushindwa kuwa na mwendelezo wa ubora, huku akiweka wazi nyota wa kigeni wanabebwa na viongozi na mashabiki.
Mpole ambaye kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kumalizana na Pamba Jiji na anahusishwa na Tanzania Prisons, amesema tayari ameanza kupokea ofa kutoka timu mbalimbali huku akiziita kufanya naye mazungumzo.
Mshambuliaji huyo aliyewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara wakati akiitumikia geita Gold, amesema kutokana na changamoto hiyo, ndiyo maana amekuwa akipambana kusaka ulaji nje ya Tanzania ili kupata thamani kubwa tofauti na ndani na wanachukuliwa kawaida.
“Ligi Kuu Bara ina wachezaji wengi wageni eneo la ushambuliaji na kati ya hao, wengi wana ubora wa kawaida lakini unapandishwa kutokana na hamasa za viongozi ili kuaminisha watu ni bora, huku sisi tukishushwa,” amesema na kuongeza;
“Wazawa tunazoeleka haraka hasa tunavyocheza timu mbalimbali za ndani. Mtu akiniona timu fulani msimu huu na ujao nyingine, ananichukulia kawaida. Kama tungekuwa tunapewa hamasa kama wageni, tungekuwa na thamani, lakini wao unakuta hata hawafungi na bado wanazungumzwa vizuri wanapewa hamasa.”
Akizungumzia kutokudumu ligi kuu ni kwa sababu ya kutokupata thamani na ameamua kutoka nje kwenda kujaribu soka la kulipwa kila apatapo nafasi hiyo.
“Inashangaza unampa kipaumbele nyota wa kigeni ambaye anakuja Tanzania kutafuta ubora, unamlipia kila kitu, wakati kuna mzawa mwenye uwezo kama wake. Wanaweza wakasajiliwa nyota watano wa kigeni na mmoja tu ndiye akawa bora na kuwa somo kwetu, lakini wengine wakawa kawaida tu,” amesema Mpole na kuongeza;
“Mshambuliaji wa kigeni anamaliza msimu mzima hana mabao kumi, huku mzawa anayecheza timu ya kawaida anafunga sawa na mgeni. Kwa nini asipewe hamasa ili awe na mwendelezo msimu unaofuata?” amehoji.
