Unguja. Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Suleiman Masoud Makame amewahimiza wananchi kuzingatia usafi wa mazingira yanayowazunguka kwani ni miongoni mwa vipaumbele muhimu vya nchi.
Waziri Makame ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Desemba 22, 2025 Mahonda, mjini Unguja alipokuwa akizindua shughuli za usafi wa mazingira ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema, usafi wa mazingira ni miongoni mwa vyanzo vikuu vinavyowavutia wawekezaji, hivyo hawana budi kuyatunza ili kuyaongezea hadhi maeneo yao.
“Ni muhimu kwa wananchi kuzingatia usafi wa mazingira yanayowazunguka kwani ni miongoni mwa vipaumbele muhimu vya nchi hasa kwa Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Mkoa wa Kaskazini Unguja ambayo ni ukanda wa uwekezaji wa utalii,” amesema.
Pia, amesema ushirikiano uliopo miongoni mwa wananchi ni kielelezo cha utekelezaji wa dhana ya mapinduzi daima, hivyo amewasihi kuyalinda na kuyaenzi.
Amesema wananchi wanapokuwa tayari kuhakikisha Mapinduzi hayo yanalindwa kwa amani na utulivu itakuwa sababu ya kuimarisha upendo, umoja na mshikamano miongoni mwao.
“Wananchi wanapaswa kutambua kuwa lengo la mapinduzi ni kuimarisha umoja, upendo na mashirikiano na leo tunaona wazi matunda yake kupitia amani na utulivu uliopo nchini,” amesema.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk Salum Soud Hamed amesema uzinduzi huo ni sehemu ya maandalizi ya shamrashamra za mapinduzi, akiwahimiza wananchi kuendelea kushikamana kwani umoja na mshikamano ndiyo lengo kuu la Mapinduzi hayo.