Serikali yatoa siku 90 wasiosajili maeneo ya kazi

Dar es Salaam. Serikali imetoa siku 90 (miezi mitatu) kuanzia Januari Mosi kwa wamiliki wa maeneo ya kazi nchini ambao maeneo yao hayajasajiliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha) kusajili maeneo hayo, kinyume na hapo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Agizo hilo la Serikali limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Oshazilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na menejimenti na watumishi wa wakala huo, leo Jumatatu Desemba 22, 2025, Sangu amesema taasisi hiyo ina dhamana ya kulinda nguvukazi ya Taifa dhidi ya ajali, magonjwa na vifo vitokanavyo na mazingira ya kazi yasiyokuwa rafiki.

Aidha, amesema ili Osha isimamie ipasavyo uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini, yanapaswa kutambulika na kupata usajili.

Mtendaji Mkuu wa Osha, Khadija Mwenda, akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, katika ofisi za Osha Dar es Salaam.

Aidha, Waziri huyo amewataka watumishi wa Osha kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kuzingatia weledi katika kuwawezesha waajiri kusimika mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi.”

“Usajili wa sehemu za kazi nchini ni kwa mujibu wa kifungu cha 16 na 17 cha Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 ambapo Osha husajili maeneo ya kazi na kisha kuyafikia kwa ajili ya ukaguzi na ushauri wa kitaalam juu ya uboreshaji wa mazingira ya kazi,” ameeleza Waziri Sangu.

Awali akizungumza, Mtendaji Mkuu wa Osha, Khadija Mwenda amesema wamepokea maelekezo ya Waziri na wako tayari kwa utekelezaji.

“Kwa niaba ya watumishi wenzangu, nikuhakikishie kwamba hatutakubali kuwa sababu ya kukwamisha utendaji wenu bali tutajitahidi kutekeleza majukumu yetu ipasavyo, na hivyo kuwafanya nyinyi viongozi wetu kutembea kifua mbele kutokana na utendaji wetu mzuri,” amesema.