Dk Mwinyi ateuwa watano, wamo wastaafu

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amewateua wakurugenzi watano kuwa wenyeviti wa bodi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kati yao wapo wastaafu wawili.

Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari leo Jumatatu Desemba 22, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, Zena Ahmed Said imesema uteuzi huo unaanza leo.

Makame Hasnuu Makame ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usafiri Zanzibar (ZMA), Makame ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Meli na Uwakala Zanzibar (Shipco).

Pia, Sultan Said Suleiman ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme la Zanzibar (Zeco), Sultan ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC).

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Burhani Mohamed ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA).

Waziri Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk Maudline Cyrus  Castico ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa).

Vilevile, Dk Idrissa Muslim Hija ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Karakana Zanzibar, Dk Idrissa alikuwa Katibu Mkuu Mstaafu wa SMZ.