TANGU yalipotangazwa makundi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 iliyoanza juzi huko Morocco, mashabiki na wapenzi wa soka nchini wamekuwa na kihoro kwa timu ya taifa, Taifa Stars wakiamini imepangwa kundi la kifo.
Uwepo wa Nigeria, Tunisia na Uganda, kumewafanya mashabiki kuwa na presha mapema, lakini unaambiwa sasa, Kocha Miguel Gamondi na wachezaji wa timu hiyo wamekula kiapo wapo Morocco kwa kazi moja tu. Kulivua joho na unyonge na leo patachimbika.
Ndiyo, kama hujui leo ikiwa imepita siku 699 ambazo ni sawa na mwaka mmoja na miezi 10 na siku 29 tangu Stars ilipocheza mara ya mwisho mechi ya michuano ya AFCON 2023 iliyofanyika Ivory Coast, timu hiyo ya taifa iliyopo Kundi C inatupa karata muhimu na mastaa wanasema’ Dijei Waletee!
Stars inashuka usiku wa leo Jumanne kutupa karata ya kwanza ya michuano hiyo ya 35 tangu ilipoanzishwa mwaka 1957 kwa kuvaana na ‘Super Eagles’ ya Nigeria, mechi itakayopigwa kuanzia saa 2:30 usiku kwa saa za Tanzania kwenye Uwanja wa Fez uliopo Mji wa Fez, Morocco ikiwa mara ya pili kwa timu hizo kukutana katika AFCON baada ya kupita takribani miaka 45.
Mara ya kwanza timu hizo zilikutana AFCON 1980 iliyofanyika Nigeria, wenyeji walipofungua kampeni kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Tanzania mjini Lagos Machi 8, 1980 kabla ya timu hiyo kwenda kubeba ubingwa wao wa kwanza wa michuano hiyo mkubwa barani Afrika.
Kwa jumla timu hizo zimekutana mara saba katika michuano tofauti, huku Nigeria ikiwa haijapoteza, ikishinda mechi nne na sare tatu, imefunga mabao 11 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu.
Stars katika mechi hizo saba dhidi ya Nigeria, ikiwa haijashinda, imeambulia sare tatu na kupoteza nne, ikifunga mabao matatu na kuruhusu 11.
Mechi zao za hivi ni za kufuzu kwa AFCON 2017, sare ya 0-0 jijini Dar es Salaam mnamo Septemba 5, 2015 kabla ya Nigeria kushinda 1-0 huko Uyo, Nigeria mnamo Septemba 3, 2016.
Kipa wa Nigeria, Amas Obasogie anayecheza Singida Black Stars iliyopo Ligi Kuu Bara, anakwenda kukutana na nyota wawili wa Taifa Stars, Hussein Masalanga na Khalid Idd ‘Gego’ anaocheza nao Singida sambamba na kocha mkuu, Miguel Gamondi anayeinoa Stars.
Ademola Lookman na Victor Osimhen, ndiyo nyota hatari wa eneo la mbele katika kikosi cha Nigeria wanaopaswa kutazamwa zaidi na mabeki wa Stars. Nyota hao ndio walikuwa wafungaji bora kikosini hapo katika kufuzu michuano hii wakiwa na mabao mawili kila mmoja. Mwingine wa kutazamwa ni Alex Iwobi na Samuel Chukwueze wanaoonekana kuwa hatari.
Kwa upande wa Stars, Simon Msuva na Feisal Salum ndio nyota waliofunga mabao mengi wakati wa kufuzu kila mmoja akipachika mawili, wakiwa ni mastaa wa kutazamwa zaidi na wapinzani bila ya kumsahau nahodha, Mbwana Samatta.
Nigeria ikiwa inashiriki AFCON kwa mara ya 21 huku ikibeba ubingwa wa michuano hiyo mara tatu 1980, 1994 na 2013, imekuwa na rekodi bora ikiiacha mbali Stars ambayo mara tatu zilizopita katika ushiriki wake wa AFCON haijawahi kushinda mechi yoyote.
Mwaka 1980 michuano ilipofanyika Nigeria, Stars ilimaliza na pointi moja, kisha haikuwa na pointi mwaka 2019 pale Misri, huku 2023 pale Ivory Coast ikimaliza na pointi mbili. Mara zote hizo ilimaliza mkiani mwa kundi.
Kwa kupata ushindi mechi ya leo, itaiweka Stars katika rekodi mpya ya kukusanya pointi tatu za kwanza katika AFCON jambo ambalo Watanzania wengi wanasubiri kuona.
Katika AFCON, Nigeria ina rekodi ya kumaliza nafasi tatu za juu kwenye fainali 13 kati ya 15 za mwisho, huku ikiwa imewahi kuishia makundi mara mbili (1963 na 1982).
Ikiwa imepoteza mechi tano pekee za kwanza katika AFCON kati ya 20, ikishinda 13 na sare mbili, Nigeria imefika angalau nusu fainali mara 13 tangu 1988. Kumbuka pia Nigeria katika AFCON tatu za mwisho haijapoteza mechi ya ufunguzi, huku pia ikipoteza mechi moja tu hatua ya makundi katika michuano 14 ya mwisho ikishinda kumi na sare tatu.
Stars ina mtihani mgumu mbele ya Nigeria kwani ukiondoa AFCON ya 1980 ilipofunga bao moja katika mechi ya ufunguzi dhidi ya wapinzani wao hao, haikurudia kufanya hivyo tena. Ilishuhudiwa mwaka 2019, mechi ya kwanza Stars ikifungwa 2-0 na Senegal, pia 2023 ikafungwa 3-0 na Morocco.
AFCON ya 1980, Stars ilifunga bao moja kila mechi kati ya tatu ilizocheza hatua ya makundi, lakini baada ya hapo, imeshindwa kurudia hilo ikishuhudiwa 2019 ikifunga mabao mawili katika mechi moja dhidi ya Kenya, kisha 2023 ikafunga bao pekee dhidi ya Zambia. Mabao hayo yalipatikana katika mechi ya pili hatua ya makundi.
Kwa sasa Simon Msuva ndiye kinara wa mabao wa kikosi cha Stars kwa AFCON akiwa nayo mawili sawa na mkongwe Thuwein Wazir aliyefunga yote AFCON ya mwaka 1980 akizifunga Misri na Ivory Coast.
Kwa upande wa Msuva mbali na mabao hayo, pia ana rekodi ya kipekee katika AFCON kutokana na kufunga fainali mbili mfululizo alizoshiriki, tena akifunga bao la kwanza si tu kwa timu yake, bali katika mechi nzima.
Alianza mwaka 2019 kufunga dhidi ya Kenya katika kipigo cha Stars ilichopokea cha mabao 3-2. Msuva alifunga bao hilo dakika ya sita, kabla ya Michael Olunga kuisawazishia Kenya dakika 39. Mbwana Samatta akiongezea Stars bao dakika ya 40.
Kipindi cha pili, Kenya ilifunga mabao mengine kupitia Johanna Ochieng Omolo dakika ya 62, kisha Olunga akafunga la ushindi dakika ya 80.
Msuva akafunga tena bao moja la Taifa Stars katika AFCON 2023 dakika ya 11 dhidi ya Zambia katika sare ya 1-1. Patson Daka aliisawazishia Zambia dakika ya 88. Bao hilo la Msuva lilikuwa pekee kwa Stars katika michuano ya mwaka huo.
Dahane Beida raia wa Mauritania aliyezaliwa Desemba 31, 1991 akiwa na miaka 33, ndiye ameteuliwa kuwa refa wa kati katika mechi hii huku akiwa na kumbukumbu nyingi zisizofutika kwa Watanzania.
Mwamuzi huyo hajawahi kuchezesha mechi yoyote ya taifa ya Tanzania, lakini amechezesha mechi nne zilizohusu klabu mbili za Tanzania, Yanga na Simba katika michuano ya CAF.
Tukio kubwa ambalo mwamuzi huyu anakumbukwa nalo na Watanzania ni lile la Aprili 5, 2024 lililozua gumzo baada ya shuti la Stephane Aziz Ki wakati yupo Yanga alilopiga dakika ya 58 dhidi ya Mamelodi Sundowns waliokuwa wenyeji wa mechi ya pili ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Afrika Kusini, kwani licha ya mpira kuonekana kudundia ndani, lakini refa huyo alikataa bao baada ya kwenda kujiridhisha kwenye VAR.
Mechi hiyo ilimalizika kwa matokeo ya 0-0 baada ya awali kushindwa kufunga pia jijini Dar es Salaam na kuamuliwa zipigwe penalti na Yanga ikapoteza kwa mikwaju 3-2.
Pia mwamuzi huyo alichezesha mechi ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya USM Alger katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyochezwa Juni 3, 2023 nchini Algeria
Kwa upande wa Simba, mwamuzi huyo ameichezesha mechi ya kwanza katika African Football League dhidi ya Al Ahly iliyomalizika kwa sare ya 2-2, Oktoba 20, 2023 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar, kisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyopigwa Mei 25, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar na kumalizika kwa sare ya 1-1.
Rekodi zinaonyesha, Beida licha ya kuonekana kuinyonga Yanga ilipocheza dhidi ya Mamelodi, lakini ndani ya muda wa kawaida hakuna klabu ya Tanzania iliyopoteza yeye akiwa mwamuzi wa kati.
Wakati Beida akiwa hajawahi kuichezesha timu yoyote ya taifa ya Tanzania, upande mwingine ameichezesha Nigeria katika fainali ya AFCON 2023 na kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Ivory Coast, Februari 11, 2024.
Mwamuzi huyo aliyeanza majukumu hayo mwaka 2018, hadi sasa amechezesha mechi 61 za mashindano tofauti ngazi ya klabu na timu ya taifa, huku akitoa kadi za njano 224 na nyekundu tano, huku penalti zikiwa 22.
Katika kundi C, baada ya Taifa Stars kucheza dhidi ya Nigeria, itafuatia mechi kati ya Tunisia dhidi ya Uganda itakayoanza saa 5:00 usiku kwenye Uwanja wa Rabat Olympic uliopo Mji wa Rabat, mwamuzi akiwa Patrice Mebiame raia wa Gabon.
Lakini kabla ya yapo, kutakuwa na mechi za kundi D zitakazochezwa mapema leo kuanzia saa 9:30 alasiri ni DR Congo dhidi ya Benin kwenye Uwanja wa Al Medina uliopo Rabat ukichezeshwa na mwamuzi Abongile Tom kutoka Afrika Kusini, kisha saa 12:00 jioni ni Senegal dhidi ya Botswana kwenye Uwanja wa Tangier uliopo Tangier.
