Dar es Salaam. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na changamoto kubwa ya kukosa utamaduni wa kujisomea.
Pamoja na kwamba elimu ni moja ya nguzo kuu ya maendeleo, Watanzania wengi hawajaweka usomaji kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku. Kwa ujumla, tabia ya kusoma nchini imeendelea kudidimia kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ukosefu wa miundombinu ya maktaba, gharama za vitabu, pamoja na mabadiliko ya teknolojia.
Ni jambo la kushangaza kuona kwamba, pamoja na idadi kubwa ya vijana wanaomaliza shule na vyuo kila mwaka, bado usomaji wa hiari nje ya masomo rasmi ni mdogo sana.
Wengi wanasoma kwa sababu ya mitihani pekee, na mara tu wanapomaliza masomo yao, wanakosa motisha ya kuendelea kujisomea.
Hali hii imesababisha Taifa kushuhudia kizazi kinachokosa tabia ya kujifunza kwa hiari, jambo ambalo linaathiri sana uwezo wa ubunifu, uelewa wa kijamii na hata maendeleo ya kitaifa.
Moja ya mambo yanayochangia hali hii ni ukosefu wa maktaba za umma za kutosha. Ni kweli kwamba kwa ngazi ya kimkoa, Tanzania imeonyesha matumaini makubwa kwani karibu kila mkoa una maktaba inayosimamiwa na mamlaka husika.
Hata hivyo, changamoto kubwa ipo katika ngazi za wilaya, tarafa, kata na hata vijiji ambapo idadi ya maktaba haivutii. Wilaya nyingi nchini hazina hata chumba achilia mbali jengo la maktaba, jambo linalowafanya wananchi, hususan vijana wa shule, kukosa sehemu ya kusomea au kupata maarifa zaidi.
Kwa mfano, mwanafunzi wa kijijini akitaka kupata kitabu cha ziada cha kujifunzia, atalazimika kusafiri umbali mrefu hadi makao makuu ya mkoa au kutumia fedha nyingi kununua vitabu ambavyo havipatikani kwa urahisi.
Hali hii inaondoa hamasa ya kusoma na inawafanya wengi kuona kama vitabu ni mali ya shule pekee, si sehemu ya maisha ya kila siku. Wakati nchi nyingine zimewekeza katika maktaba za kijamii na hata maktaba za mtandao, Tanzania bado hatujafanya vyema licha ya jitihada zilizopo zinazolenga kuleta mabadiliko.
Serikali inapaswa kutazama upya suala la ujenzi na uendelezaji wa maktaba kama chachu ya kukuza tabia ya usomaji miongoni mwa Watanzania. Maktaba si mahali pa kuhifadhi vitabu pekee, bali ni kitovu cha maarifa, ubunifu na mawasiliano ya kijamii.
Maktaba bora ni shule ya umma isiyo na ada, inayoweza kumfikia kila mtu bila ubaguzi. Hivyo, uwekezaji katika maktaba, ni uwekezaji katika elimu endelevu na maendeleo ya Taifa.
Ni muhimu pia Serikali kuimarisha taasisi zote zinazohusika na usimamizi wa maktaba nchini, kwani zimekuwa na jukumu kubwa la kuendeleza na kusimamia maktaba.
Taasisi hizi zimeonyesha kuwa na uongozi imara na wenye maono chanya kwa Watanzania. Zimebuni mikakati kadhaa ya kukuza tabia ya usomaji, ikiwemo uanzishaji wa maktaba mtandao, makongamano, maonyesho ya vitabu, kampeni za usomaji na hata ujenzi katika baadhi ya maeneo .
Hata hivyo, nikionacho taasisi hizi hazina ‘msuli’ mkubwa wa kifedha ili zifanye makubwa zaidi. Bajeti zake ndogo bila shaka ni kikwazo katika utekelezaji wa mipango yao kwa ufanisi.
Ni wakati sasa Serikali na wadau wa maendeleo kuangalia upya namna ya kusaidia juhudi za taasisi hizi. Mikakati mizuri iliyopo haitakuwa na tija ikiwa haitaungwa mkono kifedha na kisera. Bajeti ndogo inamaanisha vitabu vichache, maktaba chache, na hivyo fursa finyu kwa wananchi kusoma.
Uwekezaji katika maktaba haupaswi kuonekana kama matumizi yasiyo na faida ya moja kwa moja, bali kama uwekezaji wa muda mrefu unaojenga taifa lenye maarifa, uwezo wa kufikiri kwa kina na ubunifu wa kiuchumi.
Pamoja na juhudi za Serikali, jukumu la kukuza tabia ya kusoma halipaswi kuachiwa taasisi hizi pekee. Familia, shule na jamii kwa ujumla zinatakiwa kushiriki kikamilifu katika kuhimiza usomaji.
Wazazi wanaweza kuanza kwa kununua vitabu vya hadithi, magazeti au majarida ya elimu nyumbani ili watoto wawe na utamaduni wa kusoma tangu utotoni.
Shule, kwa upande wake, zinapaswa kutenga muda maalumu wa usomaji wa hiari bila shinikizo la mitihani, ili wanafunzi wajifunze kusoma kwa furaha na sio kwa kulazimishwa.
Aidha, katika ulimwengu wa kidijitali, kuna fursa kubwa ya kutumia teknolojia katika kukuza tabia ya usomaji. Serikali na sekta binafsi zinaweza kushirikiana kuanzisha maktaba za kidijitali ambazo zitawawezesha wananchi kusoma vitabu mtandaoni kupitia simu au kompyuta.
Hii inaweza kupunguza gharama ya ujenzi wa maktaba za majengo na kuongeza upatikanaji wa vitabu kwa watu wengi zaidi.
Kwa ujumla, ili Tanzania ijenge jamii inayopenda kusoma, lazima pawepo na mabadiliko ya kifikra na kivitendo. Serikali iweke msukumo katika ujenzi wa maktaba katika kila wilaya, isaidie kifedha taasisi zinazohusika na sekta hiyo, na kuhakikisha kwamba vitabu vinapatikana kwa urahisi na bei nafuu.
Vilevile, jamii ipewe elimu ya umuhimu wa kusoma kama njia ya kujikomboa kimaisha, kiuchumi na kifikra.
Tukumbuke kwamba taifa ambalo watu wake hawasomi ni taifa mfu. Maendeleo hayawezi kuja bila maarifa, na maarifa hayawezi kupatikana bila kusoma.
Wakati ni sasa wa kuamsha ari ya kusoma miongoni mwa Watanzania wote. Serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na wananchi kwa ujumla lazima tushikamane katika kampeni hii muhimu ya kitaifa ya kuijenga Tanzania inayosoma, Tanzania yenye kufikiri, na Tanzania yenye kujiendeleza kupitia nguvu ya elimu. 0754990083
