Wanawake kupumzika siku mbili za hedhi, kulipwa Kaunti ya Nairobi

Nairobi. Kaunti ya Nairobi imepitisha sera kwa wanawake wanaofanya kazi katika eneo hilo kupewa siku mbili za mapumziko za malipo kila mwezi kwa sababu ya afya ya hedhi nchini Kenya.

Taarifa iliyochapishwa na tovuti ya African News jana Desemba 22, 2025, imesema sera hiyo iliyoidhinishwa na Serikali ya Kaunti ya Jiji la Nairobi, imewaruhusu wafanyakazi wa kike kuchukua mapumziko wakati wa hedhi bila kuathiri likizo zao za ugonjwa wala likizo ya mwaka.

Hatua hiyo, imeibua mijadala katika mitandao ya kijamii ulimwenguni huku wachangiaji mitandaoni wakieleza kuwa imeifanya Nairobi kuwa miongoni mwa kaunti ya kwanza nchini humo kutambua rasmi hedhi kama suala halali la afya mahali pa kazi.

Mchambuzi na mchangiaji kwenye mitandao ya kijamii, Doreen Chrispian amesema, “Hatua hii ni kuhusu heshima, afya na uwazi.”

“Wanawake hawapaswi kulazimika kujifanya wako sawa ilhali wanateseka,” amesema.

Amesema wanawake wanaopata maumivu makali ya tumbo, kipandauso au uchovu uliopitiliza hali ambazo kitabibu hujulikana kama dysmenorrhea sera hiyo imeonekana kama sehemu ya kujali utu na ubinadamu sehemu ya kazi.

Hata hivyo, siyo kila mtu anayekubaliana na uamuzi huo. Wanaounga mkono sera hiyo wamesema imechelewa kwa muda mrefu. Wakosoaji, kwa upande mwingine, wanaonya kuwa huenda ikaleta madhara yasiyotarajiwa.

Baadhi ya wakosoaji wanaonya kuwa likizo ya hedhi huenda ikaendeleza dhana potofu, na kuwafanya wanawake waonekane kama wafanyakazi wasioaminika.

Wengine wana hofu kuwa sera hiyo inaweza kuathiri kwa siri maamuzi ya kuajiri, hasa katika nchi ambako ukosefu wa ajira bado ni changamoto kubwa na ushindani wa kazi ni mkali.

“Kuna wasiwasi kwamba wanawake wanaweza kupata changamoto katika kuajiri,” amesema mchambuzi mmoja, akihoji huenda sera hiyo ikawaumiza wale inaolenga kuwasaidia.

Kwa mtazamo wa kimataifa, likizo ya hedhi bado ni nadra. Nchi kama Japan, Korea Kusini na Zambia zina sera kama hizi, lakini utekelezaji na matumizi yake hutofautiana. Katika maeneo mengi, wanawake huogopa kuitumia kwa hofu ya unyanyapaa au athari hasi kazini.