Unguja. Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) limetiliana saini na Kampuni ya Central Electricals International Limited kuimarisha mfumo wa umeme mjini Unguja.
Mradi huo utagharimu Dola 17.2 milioni za Marekani (Sh42.5 bilioni), ukihusisha ujenzi wa vituo vya umeme ma mfumo wa usafirishaji nishati hiyo ndani ya Mji Mkongwe.
Akizungumza leo Ijumaa Desemba 23, 2025 baada ya utiaji saini, Meneja Mkuu wa shirika hilo, Haji Haji amesema mradi huo ni miongoni mwa hatua za uimarishaji wa Mji Mkongwe, ambako kutajengwa vituo viwili vya kupokea na kusambaza umeme, pamoja na ujenzi wa njia za kuusafirisha.
“Sehemu hii ya utekelezaji wa mradi huu itagharimu Dola 17.2 milioni (Sh42.5 bilioni) utahusisha ujenzi wa vituo vya umeme na kujenga mfumo wa kilovolti 33 wa usafirishaji umeme ndani ya Mji Mkongwe,” amesema.
Amesema kwa sasa njia za kusafirisha umeme ndani ya mji wa Zanzibar zina uwezo wa kubeba kilovolti 11. Mradi huu utajenga njia zenye uwezo wa kilovolti 33.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji Nishati na Madini Zanzibar, Joseph Kilangi amesema mkataba huo unahusu matengenezo na uimarishaji miundombinu ya umeme eneo la mjini.
Kilangi amewataka watendaji wa wizara na idara zilizo ndani ya wizara hiyo kuwasimamia wakandarasi wa mradi huo ili kuutekeleza kwa wakati.
Vilevile, ameitaka kampuni iliyopewa kazi kuitekeleza kwa ufanisi, ili waweze kupatiwa nyingine za miradi inayotarajiwa kutekelezwa na wizara hiyo badala ya kutolewa kwa kampuni za nje.
Mkurugenzi wa Miradi wa Kampuni ya Central Electricals, Hafeez Thawer ameihakikishia Serikali kuwa watatekeleza mradi huo kwa ufanisi wa hali ya juu.
Pia, ameithibitishia wizara kuwa, kampuni itawatumia Wazanzibari katika kutekeleza kazi za mradi huo.
Mradi wa uimarishaji miundombinu ya umeme ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Uimarishaji Sekta ya Nishati na Upatikanaji wa Huduma ya Umeme Zanzibar (Zesta), kujenga vituo vya kuzalisha na kusambaza umeme kwa kutumia nishati ya jua na kujenga njia za kilovolti 132.
