Upelelezi bado shtaka la mauaji ya Rhoda wilayani Serengeti

Musoma. Watu wawili akiwamo mwalimu wa shule ya msingi wamefikishwa mahakamani kwa shtaka la mauji ya Rhoda Mobe (42), mkazi wa Kijiji cha Burunga, wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara.

Washtakiwa hao ambao leo Jumanne Desemba 23, 2025 ni mara ya pili kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma ni Marco Maginga (45), ambaye ni mwalimu mkazi wa Mbeya na Mwita Maginga (45), mkulima na mkazi wa wilayani Tarime.

Kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Desemba 12, 2025 wakishtakiwa kwa mauaji ya Rhoda yaliyotokea Oktoba 23, 2025, kinyume cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kifungu cha 196 na 197.

Watuhumiwa Marco Maginga na Mwita Maginga wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma baada ya shauri lao la mauaji ya Rhoda Mobe kuahirishwa hadi Januari 5,2026. Picha na Beldina Nyakeke

Wakili wa Serikali Joyce Matindwa, ameieleza mahakama kuwa shauri hilo limefikishwa mahakamani kwa ajili ya kutajwa na kuwa upelelezi haujakamilika.

“Washtakiwa wote wawili wapo mahakamani, shauri hili limekuja kwa ajili ya kutajwa. Hali ya upelelezi bado kukamilka, tunaomba kupangiwa terehe nyingine,” amesema.

Kutokana na maelezo hayo, Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Eugenia Rujwahuka, ameahirisha shauri hilo hadi Januari 5, 2026 itakapokuja tena kwa hatua zingine.

“Shauri hili halina dhamana na mahakama hii haina mamlaka kisheria kuendesha shauri hili zaidi ya kuendesha mwenendo wa ushahidi kisha kupeleka panapohusika, hivyo naliahirisha hadi Januari 5, mwakani,” amesema hakimu Rujwahuka.