Dk Mkumbukwa: Muungano wa Tanzania ni wa kipekee duniani

Dar es Salaam. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Dk Abdallah Mkumbukwa, amesema Muungano wa Tanzania una upekee wa kipekee duniani kwa kuwa uliunganisha mataifa mawili yaliyokuwa huru,Tanzania Bara na Zanzibar umeendelea kudumu kwa zaidi ya miaka 60.

Akizungumza leo Jumanne Desemba 23, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa wasilisho kuhusu upekee wa Muungano, katika mkutano uliowakutanisha wahariri wa vyombo vya habari, Dk Mkumbukwa amesema Muungano wa Tanzania ni mfano adimu wa muungano uliodumu kwa muda mrefu licha ya changamoto mbalimbali. Mgeni rasmi katika mkutano huo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni.

Dk Mkumbukwa ameeleza kuwa nchi nyingi zilizoungana duniani, zimedumu kwa muda mfupi kutokana na malalamiko ya upande mmoja kwa madai ya kutotendewa haki.

Ametolea mfano wa nchi za Rwanda na Burundi ambazo awali zilikuwa nchi moja chini ya utawala mmoja, lakini baadaye zilitengana na hadi leo zinakumbwa na migogoro ya mipaka.

“Sudan na Sudan Kusini walikuwa nchi moja lakini walitengana. Vivyo hivyo, Jumuiya ya Afrika Mashariki ya awali iliyojumuisha Tanzania, Kenya na Uganda ilivunjika muda mfupi baada ya kuanzishwa. Tofauti na mifano hiyo, Muungano wa Tanzania umeendelea kudumu licha ya Bara na Zanzibar kutenganishwa kijiografia na bahari,” amesema.

Ameongeza kuwa upekee mwingine wa Muungano wa Tanzania ni muundo wake wa kiutawala unaounda nchi moja yenye serikali mbili, yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, kuna Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, lenye jukumu la kutunga sheria kwa masuala yanayohusu Zanzibar.

Kwa mujibu wa Dk Mkumbukwa, upekee wa tatu ni namna Muungano ulivyoanzishwa kwa amani na kwa hiari kupitia hoja na makubaliano, tofauti na miungano mingine iliyotokana na tawala za kifalme, ushindi wa kijeshi au vita.

“Muungano wa Marekani, kwa mfano, ulipitia vita vya wenyewe kwa wenyewe. Tanzania, sisi tuliungana kwa hiari, tukizingatia historia yetu na kuutangaza Muungano wetu kwa dunia,” amesema.

Amebainisha kuwa upekee wa nne ni muungano unaounganisha nchi ya bara na visiwa, hali ambayo si ya kawaida kwani mara nyingi visiwa huungana vyenyewe, kama ilivyo kwa Comoro.

“Ni nadra kwa nchi mbili kuungana na upande mmoja ukaendelea kuhifadhi utamaduni, utambulisho na kumbukumbu zake bila kuathiri Muungano. Tanzania imefanikiwa kufanya hivyo, na hilo ni jambo la kujivunia,” amesisitiza.

Kwa upande wake, mkurugenzi mstaafu wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Salvatory Rweyemamu, aliwataka wahariri na wadau wa habari kuacha ushabiki katika uandishi wa habari zinazohusu Muungano wa Tanzania.

Amesema Muungano huo ulianzishwa na wazalendo kwa misingi ya ukweli na masilahi mapana ya Taifa.

Rweyemamu amesema ushabiki hauna tija wala faida kwa Taifa, na akaeleza umuhimu wa kuandika habari kwa kuzingatia ukweli, taaluma na uwajibikaji wa kitaaluma.

“Tuwe waangalifu na tuache ushabiki. Ukivunjika Muungano hakuna faida yeyote tutakayopata. Tuandike habari za Muungano tukizingatia ukweli na maadili ya taaluma,” amesema Rweyemamu.

Ameongeza kuwa Tanzania Bara na Zanzibar zina uhusiano wa muda mrefu wa kihistoria, kijamii na kiutamaduni, akibainisha kuwa wananchi wa pande zote mbili wameoleana na kushirikiana katika nyanja mbalimbali za maisha, hali inayozidi kuimarisha mshikamano na umoja wa Taifa.