2025 ilivyoacha tabasamu na vilio kwa mastaa

Mwaka Mpya wa 2026 unasubiriwa kwa shauku kubwa wakati huu wa 2025 ukiwa ukingoni ukiacha mambo mengi nyuma.

Kwenye burudani, mengi mazuri kwa maana ya kufurahisha yalitokea, pia ya kuhuzunisha na kubaki katika kumbukumbu za baadhi ya mastaa.

Hawa hapa mastaa ambao mwaka huu uliobakiza siku nane kumalizika umewaacha kwenye furaha na huzuni katika uhusiano wa kimapenzi na mambo mengine.

Hawa ni wasanii ambao waliweka wazi uhusiano yao Februari 14, 2021 Siku ya Wapendanao na ulidumu kwa mwaka mmoja ukavunjika 2022 kwa tuhuma za usaliti.

Ilikuwa Aprili 2022 pale penzi lao liliposambaratika baada ya kuvuja kwa picha chafu ambazo Harmonize ilielezwa alimtumia mtoto wa Kajala, Paula.

Juni 2022, walwili hao walisameheana, wakarudiana na kuvishana pete ya uchumba, katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, hafla uliyohudhuriwa na baadhi ya watu wao wakaribu.

Ilipofika mwaka 2023, Harmonize na Kajala waliachana tena! Hii ndio ilikuwa ya moto, Harmonize alifuta tattoo aliyomchora Kajala na kufuta utambulisho wa umeneja wake, huku Kajala akifuta picha za kuvishwa pete na nyingine za Harmonize katika kurasa zao za mitandao ya kijamii.

Mwaka huu wa 2025, ziliibuka habari kuwa wamerudiana baada ya kusambaa kwa video ya wawili hao wakikumbatiana katika mashindano ya soka ya Samia Cup. Stori zilidai wamerudiana japo Kajala anafanya kwa kujificha sana kwa sababu hapendi kumkera bintiye, Paula, anayesemekana hataki kusikia kuhusu uhusiano huo.

Habari ziliendelea kudaiwa kuwa wamerudiana kutokana na kuonyesha kila dalili katika sherehe ya kuzaliwa mtoto wa Marioo na Paula.

Hadi sasa mashabiki wa nyota hao wameshindwa kuelewa iwapo wawili hao wamerudiana kweli au walikuwa wanazuga tu kwani hakuna ambaye amekuwa tayari kuweka wazi jambo hilo, ingawa katika ‘birthday party’ hiyo ya mwaka mmoja wa kuzaliwa wa mtoto Amara, walionekana wakiwa katika mahaba mazito.

Mkali huyu mwingine wa zamani wa Lebo ya WCB amejikuta 2025 akionja chungu baada ya kutengana na mwandani wake, Fahyma ambaye ni mama wa mtoto wake wa kiume aitwaye Jaydan.

Ilisemekana kuwa, chanzo cha wawili hawa kutengana ni kitendo cha usaliti na kila mmoja akimtuhumu mwenzake kuchepuka. Na hiyo sio mara ya kwanza kwa wawili hao, huwa wanachana na kurudiana kila wakati.

Wolper na Rich Mitindo walifunga ndoa Novemba, 2022 katika Kanisa la St. Peter’s lililopo jijini Dar es Salaam.

Baadaye, mwanzoni mwa mwaka huu 2025, Wolper alitangaza kuachana na Rich kwa madai ya kusalitiwa, huku stori za mitaani zikidai kwamba mwanaume huyo alikasirishwa na tuhuma zilizomuandama Wolper kwamba jumba la kifahari wanaloishi wawili hao, amejengewa na kiongozi mmoja wa kiimani.

Ilipofika Februari 2025, Wolper alithibitisha kurudiana na mume wake Rich Mitindo, baada ya takribani mwezi mmoja uliotangulia kuujuza umma kupitia ukurasa wake wa Instagram kwamba ameachana na mfanyabiashara huyo wa nguo.

Na hata hivyo kwasasa kuna madai ya kuwa wawili hao hawako vizuri tena kwenye ndoa yao kwamba kilichobaki zaidi ni kuleata watoto, japo wenyewe hawajaweka wazi suala hili.

Mwaka huu 2025 unaweza kusema haikuwa bahati kwa waliokuwa wakipendana, Haji Manara na mwigizaji Zaiylissa.

Wawili hao walianza kurushiana maneno kwenye mitandao ya kijamii wakionyesha penzi lao si penzi tena bali ni majanga huku Manara akisema hiyo siyo kiki bali ndiyo uhalisia wa kinachoendelea baina yao kuwa ndoa yao imevunjika.

Manara na Zaylissa walifunga ndoa Januari 24, 2024 huku ikiwa ni ndoa ya sita kwa Manara na ya pili kwa Zaiylissa. Aprili 2025 ndoa hiyo ilikuja kuvunjika.

Kwa upande wa msanii huyu wa Bongofleva, Darassa, yeye ameonja tamu na chungu mwaka huu wa 2025. Utamu ni baada ya kuachia albamu yake mpya inayokwenda kwa jina la Take Away The Pain ikiwa na nyimbo 15.

Na ikumbukwe Darassa kutokea Classic Music Group (CMG), hii ni albamu yake ya pili baada ya kutoa, Slave Become A King (2020).

Kwenye chungu ni pale Darassa mwaka huu 2025, Jun 21, alipofiwa na mama yake mzazi na mazishi yalifanyika nyumbani kwao Itigi mkoani Singida.

Ni msanii wa Bongo Movies, mwaka huu wa 2025 hali yake kiafya haikuwa nzuri.

Wastara tumbo lilimvimba, ngozi ikababuka na pia kwa mujibu wake anaeleza kuwa kuna madhara ameyapata kwenye ini. Na chanzo cha yote, anadai kuwa ni kuwekewa sumu na wabaya wake.

Msanii wa singeli Meja Kunta, Aprili 14, 2025 alipata chungu baada ya kufiwa na mama yake mzazi Mosi Mkalawile aliyefia mkoani Lindi wakati alipokwenda kufanya biashara zake za samaki, kuzikwa kwenye makaburi ya City Yombo Wilayani Temeke.